Michezo

KSG Ogopa inavyowaangamiza mahasidi ligini

May 22nd, 2018 2 min read

Na PATRICK KILAVUKA

MELI ya timu ya kandanda ya Kenya School of Government (KSG Ogopa) iling’oa nanga kwa kishindo baada ya kupata kocha na wachezaji wa kujituma zaidi.

Imesajiliwa katika ligi ya FKF, Kauntindogo, Tawi la Nairobi Magharibi kama njia ya kukuza vipaji vya utajiri wa soka.

Katika mchuano wake wa kwanza, ilianza na heri baada ya kuishinda FC Talent 1-0 kwenye mpepetano wa kusisimua uwanjani Kihumbuini.

Kikosi cha timu ya kandanda ya Kenya School of Government (KSG Ogopa). Picha/ Patrick Kilavuka

Bao la mtikisa nyavu Seby Kivairo liliwaacha wapinzani vinywa wazi na hivyo basi, kuifungulia milango kuchukua pointi tatu. Isitoshe, imeashiria kwamba, azma yake ya kuwa na jicho pevu ligini ipo.

Fauka ya hayo, imejiongezea matumaini kwa kuiliza Parklands Sports Club 2-0 katika mechi yake ya pili ya ligi hiyo kabla kuwazima watani wao Karura Green 4-1 katika mchuano wa kirafiki.

Kufikia ufanisi huo ligini, ilipiga mechi za kujipima nguvu dhidi ya Moyale kutoka Eastleigh na kuichuna 3-0,Tebeka FC na kuilima 4-0, Kabete Cares na kuiyeyusha 1-0.

KSG Ogopa ikifanya mazoezi. Picha/ Patrick Kilavuka

Matokeo mengine  ya michuano hiyo yalikuwa sare mbili za 2-2 dhidi ya Terror Squad na White Eagles uwanjani KSG, Lower Kabete kabla kuagana tena na Kariobangi FC  2-2, uwanjani Lucky Summer.

“Tunaamini kwamba azimio letu liko wazi kwani, tunapania kuwa timu bora baada ya kumpata kocha na kutufaa kwa maandalizi ya ligi.

Isitoshe, timu imeanza kuonesha dalili za kuimarika zaidi na tayari tunashiriki ligi yenye ushindani mkali na tunanuia kucheza tu msimu huu ligini kisha tukwea Kaunti,” aeleza timu meneja Gordon Odwar.

Anashirikiana na kocha mpya Nicondemus Kefa na meza ya kiufundi chini ya naibu wa kocha Peter Muturi, katibu mkuu Marvia Imbali, mshirikishi wa timu Yakub Mohammed na katibu mpanga ratiba Erick Bulogosi Mulama.

Wachezaji washauriana kuhusu mbinu bora za kupata ushindi. Picha/ Patrick Kilavuka

Kujitolea kwa wasimamizi wa shule hii wakiwemo mkurugenzi mkuu Daktari Ludeki Chweya, mkurugenzi wa masuala ya Usimamizi na Fedha Daktari Nura Mohammed na mkurugenzi wa Maendeleo na Masomo Bw Humphrey Mokaya, umeipelekea timu hii ya wachezaji 22 kuwa na ari ya kuhakikisha jina la Shule ya Serikali linawekwa kwenye ramani ya michezo na kuwawezesha vijana kuwa na uwezo wa kukuza vipawa vyao kutimiza mojawapo wa ajenda nne za Serikali Kuu.

Timu hii, imejumuisha wafanyakazi wa shule hii, wanachuo wa Lower Kabete na vijana wenye vipaji vya soka.
Hata hivyo, wanasoka ambao hawajaajiriwa na wana vipaji, wanatarajia kuwa na muafaka wa kufanya kazi za vibarua au za ofisi pindi muafaka utaafikiwa ili, wawe pamoja kuimarisha timu.

“Baada ya kazi, tungependa waelekea uwanjani kujinoa,” wanakariri wadau wa timu.

Mazoezi yachacha. Picha/ Patrick Kilavuka

Mipango? Ni kutua ligi za hadhi nchini, angalau wanasoka wapate ajiri, wanatalanta kuhamasishwa kuhusu programu za vijana na kuwapelekea kuwa na uwezo wa kuwajibika katika jamii.

Isitoshe, kusisitiza nidhamu kama nguzo ya mchezaji na kuwaepusha na visa dhidi ya utovu wa usalama na mihadarati ili, watimize malengo ya Serikali Kuu kuhusu kuwapa vijana uwezo wa kuibua mikakati na maazimio yao ya ruwaza ya 2030.

Changamoto yao sasa ni muda wa kujinoa na kujifahamisha na ligi wanayoshiriki, huu ukiwa ni msimu wao wa kwanza.

Kama timu, wanashukuru wasimamizi wa shule kwa usaidizi wa hali na mali ambao umeikumbatia  timu na kuiwezesha kustawisha talanta pamoja na kushiriki ligi.