Michezo

KSG Ogopa yabanwa na Dagoretti Lions

February 10th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya KSG Ogopa FC ilipigwa breki ilipozabwa bao 1-0 na Dagoretti Lions kwenye mechi ya kuwania taji la Nairobi West Regional League (NWRL) iliyochezewa uwanja wa Shule ya Upili ya Dagoretti High, Nairobi.

Nayo Kibera Saints ilitandika KFS mabao huku WYSA United ikitoka chini baada ya kupigwa bao 1-0 na kutwaa ushindi wa mabao 3-2 mbele ya Uthiru Vision.

Wachezaji wa KSG Ogopa na Dagoretti Lions walionyesha upinzani wa kufa mtu huku pande zote zikitafuta ufanisi wa alama tatu muhimu.

Licha ya kocha, Peter Mutwiri wa KSG Ogopa kufanya mabadiliko kadhaa bahati haikusimama bali mwishowe walikubali yaishe baada ya kudungwa bao hilo lililojazwa kimiani na Pius Omachi ndani ya kipindi cha pili.

”Bila shaka nashukuru vijana wangu walijitahidi kiume kukabili wapinzani wao na hatimaye bahati ilisimama na kujiongezea pointi tatu muhimu na kurukia uongozi wa kampeni za muhula huu ingawa wapinzani wetu wanakuja kivingine,” alisema kocha wa Dagoretti Lions, Joseph Makokha na kuwataka vijana hao kutolaza damu bali wazidi kujituma kwa udi na uvumba kupigania taji la msimu huu.

Nayo Kibera Saints ya kocha, William Mulatya iliyoshikilia nafasi ya kwanza kwa muda ilipata mabao hao kupitia juhudi zake Enock Omosa alipocheka na wavu mara mbili.

Nayo WYSA ilishusha soka safi na kuzoa mafanikio hayo kupitia Kelvin Etemesi, Theophilas Simango na Laktano Kiprotich waliofunga bao moja kila mmoja.

Nayo Uthiru Vision itajilaumu vikali baada ya mchezaji wake, Stephen King’ori kujikuta macho kwa uso mara tatu na kipa wa WYSA, Kelvin Wachira lakini wapi alishindwa kufunga.

”Nashukuru kikosi changu kinazidi kujitahidi ila kiasi safu ya kiungo cha kati inaonekena kutomakinika lakini nahifanyia kazi,” alisema kocha wa WYSA, Turncliff Asiebella na kuongeza kuwa wamepania kukaza buti kufukuzia taji la msimu huu na kutwaa tiketi ya kupandishwa ngazi.

Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, Caleb Sisco na Ryna Kariuki walifungia Parklands Sports na Kibera Soccer mtawalia na kusaidia kutoka sare ya bao 1-1.

Kibera Lexus iliagana sare tasa na Kemri, Maafande wa Nairobi Prisons walituzwa ushindi wa mezani baada ya Ligi Ndogo kuingia mitini, nao Wilson Anguli na William Owade kila mmoja alicheka na wavu mara moja na kubeba South B United kuzoa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Uweza FC.

Matokeo hayo yamefanya, Dagoretti Lions kutwaa uongozi wa kipute hicho kwa alama 27, sawa na Kibera Soccer tofauti ikiwa idadi ya mabao.

Nao wapigagozi wa KSG Ogopa wanafunga tatu bora kwa alama 26, moja mbele ya Kibera Saints. Nacho kikosi cha Maafande wa Nairobi Prisons kimetua tano bora kwa kuvuna alama 23, moja mbele ya WYSA United ambayo ina mechi mbili kapuni.