Michezo

KSG Ogopa yazidi kupepea ligini

February 3rd, 2020 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Parklands Sports iliikandamizwa kwa magoli 10-0 na wachezaji wa KSG Ogopa FC kwenye mechi ya kuwania taji la Nairobi West Regional League (NWRL) iliyopigiwa uwanja wa KSG.

Nayo Kibera Saints iliitandika KYSA Karengata mabao 3-0 na kujiongezea matumani ya kusonga mbele huku Uweza B ikidungwa bao 1-0 na Dagoretti Lions.

Saints iliingia mzigoni kwa machungu ambapo ilijituma kisabuni na kufanya kweli siku chache baada ya kutoka sare tasa na Ligi Ndogo.

Wanasoka hao waliteremsha mechi safi na kuzima ndoto ya wapinzani wao pale Enock Omosa alipotikisa wavu mara mbili huku David Omoro akifunga mara moja.

”Tunashukuru Mola kwa ushindi huo maana kampeni za muhula huu hakika zinazidi kupamba moto,” alisema kocha wa Saints, William Mulatya. Nayo Kibera Lexus ilikung’utwa magoli 3-1 na AFC Leopards Youth baada ya Vincent Nyadondi kufunga mara mbili naye Brian Bwire alitupia kambani bao moja.

Silver Bullets iliendelea kutembeza vipigo mbele ya wapinzani wao iliporarua KFS mabao 2-1. Denis Munyao na Collins Mumasi kila mmoja alipiga kombora moja safi na kubeba Silver Bullets kutia kapuni alama zote siku chache baada ya kunyamazisha South C United kwa mabao 3-1.

Nao Maafande wa Nairobi Prisons waliibuka wepesi waliponyukwa mabao 3-2 na Mt Kenya University (MKU) Nairobi huku Kibera Soccer ilibeba mabao 3-1 dhidi ya Ligi Ndogo.

Kwenye jedwali la kinyang’anyiro hicho, KSG Ogopa FC inayoshiriki michezo hiyo kwa mara ya kwanza ingali kileleni kwa alama 26 sawa na Kibera Soccer tofauti ikiwa idadi ya mabao.

Picha/JOHN KIMWERE

Kocha wa Kibera Lexus, David Owino akiongea na vijana wake kabla ya kushuka dimbani kukabili South B United kwenye mechi ya Nairobi West Regional League(NWRL) ugani Woodley Kibera, Nairobi. Mechi ilikamilika sare ya mabao 2-2.