KTDA yabishana na Rais kuhusu chaguzi za wakuu viwandani

KTDA yabishana na Rais kuhusu chaguzi za wakuu viwandani

Na CHARLES WASONGA

MALUMBANO yamezidi kutokota kati ya Serikali na Shirika la Kustawisha Sekta ya Majani Chai Nchini (KTDA), kuhusu suala la kufanyika kwa chaguzi za wakurugenzi wa viwanda vya majani chai kote nchini.

KTDA imezidi kushikilia msimamo wake wa kupinga chaguzi, licha ya Rais Uhuru Kenyatta kuamuru, kupitia Agizo Rasmi alilotoa Machi 12, kwamba Bodi ya Chai Nchini (KTB) iendeshe chaguzi hizo ndani ya siku 60.

Hii, akasema Rais, ni sehemu ya mageuzi katika sekta hiyo yanayolenga usimamizi wake kwa manufaa ya wakulima.

Huku KTDA ikisema chaguzi hizo hazifai kuendelea kutokana na kuwepo kwa agizo la mahakama lililozisimamisha mwaka jana, Waziri wa Kilimo Peter Munya, jana alisema kuwa agizo hilo halikushirikisha viwanda 69 vya majani chai.

Kulingana na Waziri huyo viwanda hivyo viko huru kuendelea na chaguzi za wakurugenzi wapya kwani KTDA na maajenti wake, ndio walizuiwa kusimamia chaguzi hizo, kulingana na agizo hilo lililotolewa na Mahakama Kuu ya Nairobi.

“Agizo la mahakama katika kesi nambari 87 ya 2020 limebainisha wazi kwamba ni KTDA kama wahusika wakuu, maajenti au wateule wake, ambao walizuiwa kuendesha chaguzi zozote za wakurugenzi. Viwanda vyote 69 ambavyo ni huru kulingana na Sheria za Kampuni, havikuzuiwa kuendesha chaguzi zao,” Bw Munya akasema kwenye taarifa iliyochapishwa katika toleo la Jumatano la gazeti la Daily Nation.

“Viwanda hivyo, havikushirikishwa katika kesi hiyo kati ya KTDA na Chama cha Wafanyabiashara wa Chai Afrika Mashariki. Kwa hivyo, viwanda hivyo vinaweza kuendelea na chaguzi za wakurugenzi bila kusimamiwa na KTDA,” akaongeza.

Lakini katika taarifa kwa vyombo vya habari, KTDA inashikilia kuwa agizo hilo la mahakama linasimamisha chaguzi za wakurugenzi ambazo zilikuwa zimeratibiwa kufanyika mwaka 2020.

“Agizo la mahakama linalosimamisha chaguzi za wakurugenzi wa viwanda vya majani chai lingalipo. Agizo hilo lilitolewa na Mahakama Kuu ya Nairobi, ambayo ilijumuisha kesi mbili zilizowasilishwa Mombasa na Nairobi,” ikasema.

Kulingana na KTDA, Sheria za Kampuni zinasema kuwa ni kampuni husika zenyewe mamlaka ya kuitisha na kuendesha mikutano na chaguzi wala sio wala sio asasi zingine au serikali.

“Kwa hivyo, serikali, wizara ya kilimo au asasi zake kama vile Bodi ya Chai Nchini hazina mamlaka ya kuitisha, kuendesha au kusimamia chaguzi za wakurugenzi wa viwanda vya majani chai,” KTDA ikaeleza.

Lakini Bw Munya alikana madai hayo akisema wajibu wa serikali katika shughuli hiyo ni kutoa ushauri na mazingira salama kwa viwanda hivyo kuendesha chaguzi zao, bali “sio kuendesha na kusimamia chaguzi zenyewe.”

“Kwa hivyo Mheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta na Wizara ya Kilimo wametoa ushauri na kutoa usalama kwa viwanda hivi kufanya chaguzi kuhakikisha kuwa vinaafiki sheria. Ikiwa vitafeli kufanya chaguzi vitapewa adhabu kali kwa mujibu wa Sheria za Kampuni,” akasisitiza Bw Munya.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Muungano wa Wadau katika Sekta ya Majani Chai, Bw Irungu Nyakera, ameunga mkono msimamo wa serikali katika suala hili, akiisuta KTDA kwa kutaka kuendelea kunyanyasa wakulima kwa kudhibiti chaguzi za wasimamizi wa viwanda vya majani chai.

“KTDA ilisimamia chaguzi zilizojaa udanganyifu mnamo 2019 na ambazo zilifutiliwa mbali na mahakama. Sasas baada ya Rais Kenyatta kutia saini kwa Mswada wa Chai kuwa sheria, sasa wakulima 600,000 wameanza mchakato wa kusimamia sekta hiyo. Hii ni kupitia chaguzi za wakurugenzi wa viwanda vya majani chai,” akasema Bw Nyakera, ambaye zamani alihudumu kama Katibu katika Wizara ya Uchukuzi.

Wakati huo huo, wakulima wa majani chai katika eneo la Mlima Kenya wanaendelea na mchakato wa chaguzi za wakurugenzi wa viwanda licha ya pingamizi kutoka kwa KTDA.

You can share this post!

CORONA: Uwezo wa chanjo ya China katika kuisaidia Afrika...

Walimu watakaosahihisha KCPE watakuwa katika mazingira...