Habari Mseto

KTDA yapinga agizo la hesabu zake kukaguliwa

October 29th, 2019 2 min read

Na NDUNGU GACHANE

MAMLAKA ya Ustawishaji wa Majani Chai (KTDA), imewasilisha ombi la kuitaka mahakama isitishe amri iliyoruhusu mkaguzi wa hesabu kuchunguza akaunti za asasi hiyo, ikisema haimilikiwi na serikali.

KTDA iliwasilisha ombi hilo katika mahakama ya Murang’a baada ya serikali ya kaunti kushinda kesi na korti kuamrisha vitabu vya hesabu vya halmashauri hiyo vya mwaka 2018, vikaguliwe kufuatia kudorora kwa bonasi ya wakulima.

Kupitia wakili, Bw Mwangi Kibicho, KTDA ilisema kwamba afisi ya mkaguzi mkuu ni asasi huru na iliyotwikwa jukumu la kuchunguza na kutoa ripoti kuhusu mashirika ya serikali ambayo hufadhiliwa na fedha za umma.

“Mshikilizi wa afisi ya mkaguzi wa hesabu anafaa kutekeleza wajibu wake bila kuingiliwa. KTDA ni shirika la kibinafsi na mkaguzi wa hesabu hana jukumu la kuingilia utendakazi wake kulingana na katiba,” akasema Bw Kibicho.

KTDA vilevile ilishutumu serikali ya Kaunti ya Murang’a kwa kutumia suala hilo kutimiza maslahi ya kisiasa kupitia korti, akitaja tabia hiyo kama kutumia mahakama vibaya.

KTDA pia imeomba mahakama kuunganisha kesi hiyo na ile iliyowasilishwa katika mahakama ya Kericho ambapo Kaunti ya Murang’a imejumuishwa huku ikiomba isikizwe na jopo la majaji watatu watakaochaguliwa na Jaji Mkuu hadi ikamilike.

Gavana wa Kericho, Bw Paul Chepkwony aliwasilisha kesi ya wakulima 400,000 wa mashamba madogo kutoka kulipwa fidia kwa kunyanyaswa kibiashara na wafanyabiashara walaghai katika sekta ya majani chai.

Bw Chepkwony pia alitaka mahakama ya Kericho iamrishe KTDA iwarudishie wakulima Sh87 bilioni kutoka ukanda huo kwa kuwatoza mara mbili ada ya usimamizi huku akishtumu mamlaka hiyo kwa kusimamia vibaya sekta ya majani chai na kuchangia malipo duni kwa wakulima hao wa mashamba madogo.

Ombi kusikizwa

Hata hivyo, Jaji wa mahakama kuu aliamrisha kwamba ombi lililotaka kesi hiyo isikizwe na jopo la majaji watakaoteuliwa na Jaji Mkuu, litasikizwa na liamuliwe kwanza kabla ya maombi mengine kuzingatiwa na korti.

“Wawakilishi wa pande zote wamekubaliana kwamba lazima tusikize na kuamua kuhusu ombi la kesi kusikizwa na majaji watakaoteuliwa na Jaji Mkuu na ninatangaza Novemba 29 kama siku ya kusikizwa ombi hilo,” akaamuru Jaji.

Gavana wa Murang’a, Bw Mwangi Wa Iria ambaye alidhamini kesi hiyo alisema kwamba wakulima pia wanataka kujumuishwa na atapinga juhudi zozote za kuihamisha hadi Nairobi.

“Kwa nini KTDA inakataa kufanyiwa ukaguzi? Kwa nini wanataka kesi hiyo ihamishwe hadi Nairobi? Tutauliza maswali haya huku wakulima pia wakituma ombi la kujumuishwa kwenye kesi,” akasema.

Wiki iliyopita, Bunge la Kaunti ya Murang’a pia lilituma ombi la kujumuishwa kwenye kesi hiyo.