Michezo

KU na MKU zatamba voliboli ya vyuo vikuu

February 25th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) City ya wanaume na wanawake wa Mt Kenya University (MKU) kila moja ilivuna pointi sita muhimu kwenye kampeni za ligi ya voliboli ya vyuo vikuu nchini (KUSA) kanda ya Kaskazini.

Wanaume wa (KU City) walitwaa pointi sita muhimu waliponasa ufanisi wa mechi mbili kwa seti 3-0 kila moja dhidi ya wenzao wa Gresta na Pan African University (PAC). Wanaume hao walibeba ushindi wa alama za 25-15, 25-21, 25-22 mbele ya Gresta kisha kutuzwa alama za 25-0, 25-0, 25-0 bila jasho ikiwa ni ushindi wa mezani baada ya wapinzani wao PSC kuingia mitini.

Kwa wanawake, MKU ilichota alama sita muhimu baada ya kulaza Daystar na KU City seti 3-0 kila moja. Warembo hao walibeba alama za 25-07, 25-17, 25-23 mbele ya Daystar University kabla ya kubamiza KU City kwa alama za 25-12, 25-12, 25-16.

Kwenye matokeo mengine ya mechi hizo kwa wanaume, St Paul University (SPU) ilinasa alama tatu bila jasho seti 3-0 (25-0, 25-0, 25-0) dhidi ya Daystar University. Timu hiyo ilipiga hatua ilipozoa ushindi wa mezani baada ya wapinzani hao kuingia mitini. Nayo timu ya Kenya Kenya College of Accountancy (KCA) ilipepeta MKU seti 3-2 kwenye patashika iliyoshuhudia msisimko mkali. Madume hao waliandikisha ufanisi wa alama za 20-25, 25-19, 25-20, 23-25,15-09.

Kwenye mfululizo wa kipute hicho upande wa kina dada, wachezaji wa KCA walijikuta njia panda walipokiri kichapo cha seti 3-0 mikononi mwa SPU. Wanazuo wa SPU waliendeleza ubabe wao kufuata waliowatangulia waliporarua wapinzani wao kwa alama za 25-09, 25-18, 25-11. KCA iliyeyusha mchezo wa pili na kulazimika kuondoka mikono mitupu baada ya kukubali kulala kwa seti 3-0 mbele ya JKUAT. Nayo KU City iliandikisha ufanisi wa seti 3-0 (25-16, 25-12, 25-21) dhidi ya Gresta.