Habari MsetoSiasa

Kubali yaishe, Ruto aambiwa

November 14th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa Jubilee wanaoegemea mrengo wa handisheki wamemtaka Niabu Rais William Ruto kukubali kushindwa kwa mgombeaji wa chama hicho McDonald Mariga katika uchaguzi mdogo wa Kibra.

Pia wamemtaka akome kuingiza jina la Waziri wa Usalama, Fred Matiang’i katika siasa za Kibra.

Wakiwa wameandamana na wenzao wa ODM, wabunge hao walisema madai ya wabunge wa ‘Tangatanga’ kuwa Dkt Matiang’ i, Katibu wa Wizara hiyo Karanja Kibicho na Kiongozi wa ODM Raila Odinga walikutana kupanga fujo hayana ukweli wowote.

Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kiambu, Gathoni Wa Muchomba alisema Dkt Ruto na wabunge wandani wake wanatafuta kisingizio cha kupinga ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI).

“Tungependa kumshauri Naibu Rais na wenzake wakubali kuwa walishindwa katika uchaguzi wa Kibra na wakome kuwalaumu watumishi wa umma ambao hawakuhusika kwa njia yoyote katika uchaguzi. Pia wajue kwamba tutawashinda tena ripoti hiyo itakapowasilishwa bungeni,” akasema Bi Wamuchomba.