Michezo

Kubwa zaidi katika ndoto zangu ni kuchezea Real Madrid – Pogba

October 9th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KIUNGO Paul Pogba wa Manchester United amekiri kwamba kubwa zaidi katika maazimio yake kitaaluma ni kuchezea Real Madrid ya Uhispania kabla ya kustaafu soka.

Hata hivyo, Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 27 amesisitiza kwamba kwa sasa analenga “kila kitu kinachowezekana” kuhakikisha kwamba Man-United wanarejea “wanakostahili” kuwa kwenye soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na bara Ulaya.

Pogba amekuwa akihusishwa mara kwa mara na uwezekano wa kusajiliwa na Real Madrid tangu ajiunge upya na Man-United kutoka Juventus kwa kima cha Sh12 bilioni mnamo 2016.

Ingawa mkataba wa sasa kati ya Pogba na Man-United unatarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21, huenda kocha Ole Gunnar Solskjaer akarefusha zaidi muda wa kuhudumu kwa nyota huyo ugani Old Trafford kwa mwaka mmoja zaidi hadi 2022.

Katika mahojiano yake na gazeti la Mirror Sport nchini Uingereza, Pogba ameungama kuwa hajaanza mazungumzo yoyote na Real Madrid kuhusu mipango ya kumsajili japo azma yake ni kustaafu soka akivalia jezi za miamba hao wanaonolewa na kocha Zinedine Zidane.

Man-United wameanza vibaya kampeni za msimu huu katika EPL ambapo wamesajili ushindi mara moja pekee kutokana na mechi tatu za ufunguzi dhidi ya Crystal Palace, Brighton na Tottenham Hotspur.

Baada ya kupokezwa kichapo cha 3-1 kutoka kwa Palace, Man-United walijinyanyua dhidi ya Brighton kwa kuwapepeta 3-2 kabla ya Tottenham kuwaponda 6-1 katika mechi yao ya mwisho ya EPL uwanjani Old Trafford mnamo Oktoba 4, 2020.

Pogba amepangwa katika kikosi cha kwanza cha Man-United katika mechi zote tatu zilizopita msimu huu baada ya kupona Covid-19 mnamo Agosti 2020.