Bambika

Kuchapa baada ya kuachana na Mulamwah kulifanya niende VCT – Carrol Sonie

February 21st, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MWIGIZAJI Caroline Muthoni Ngethe almaarufu Carrol Sonie amezungumzia jinsi alivyokabiliana na msongo wa mawazo uliosababisha mabadiliko ya mwili wake baada ya kuachana na mchekeshaji David Oyando almaarufu Mulamwah.

Mwigizaji huyo alikiri kuathirika kisaikolojia kiasi kwamba alilazimika kutafuta usaidizi wa mtaalamu.

Kulingana na mama huyo wa mtoto mmoja, kila akijiangalia kwa kioo, aliona muonekano wake ukiwa sawa hadi pindi tu baadhi ya mashabiki walianza kuibua maswali na minong’ono.

“Wakati huo nilikuwa nimekonda na kuna mtu aliniuliza ‘Sonie kwani una Ukimwi?’. Nilikuwa nimekonda. Kusema kweli niliulizwa swali hilo hadi nikaamua kuenda kupimwa licha ya kwamba nilijua tu vizuri sina mdudu,” akafunguka Sonie.

Hata hivyo alimshukuru mwanasaikolojia wake akifichua kwamba alimsaidia kukabiliana na msongo wa mawazo.

“Nadhani kwa kweli nilienda kwa mtaalamu bora katika ulimwengu huu. Alinisaidia sana kujijua na kujielewa. Sidhani kuna kitu kinaweza kunirudisha nyuma hadi mahali ambapo nilikuwa. Kipindi hicho nilikuwa nakula sana lakini siongezi uzani,” akafichua mwigizaji huyo

Mwigizaji huyo mapema juma hili alisema kuwa amerejelea kazi yake kwenye Chaneli ya YouTube akiwa na lengo la kupata mapato.

Miaka miwili iliyopita, alikiri matukio ya kukosa kunyonyesha mtoto na kula zaidi ilikuwa ni chanzo cha dalili ya msongo wa mawazo.

Wakati huo, alikiri kumpeza sana Mulamwah katika safari ya kumlea binti yao, jambo ambalo kwa sasa ni tofauti.