Habari za Kaunti

Kuchonga muguka sasa ni haramu Mombasa

May 24th, 2024 1 min read

NA KEVIN MUTAI

SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa sasa imepiga marufuku usafirishaji na matumizi ya muguka ndani ya kaunti hiyo.

Gavana Abdulswamad Nassir, alitoa amri kwamba maduka yote yanayouza bidhaa hiyo yafungwe mara moja, akataka maafisa wa usalama wa kaunti pia wazuie magari yatakayopatikana yakijaribu kusafirisha muguka katika jiji hilo.

Hatua hii inajiri wakati ambapo utawala wa kaunti hiyo inazidi kuchukua hatua kali za kudhibiti utafunaji muguka na miraa, ikisemekana uhuru uliopo umefanya watoto wa shule kujiingiza katika uraibu huo.

Kulingana na Bw Nassir, amri yake imetolewa kwa msingi wa sheria zinazoipa serikali ya kaunti mamlaka ya kusimamia utoaji leseni za kibiashara.

Alisema alizingatia maslahi bora ya umma kutokana na maoni yaliyopokewa kwenye mashauriano na wananchi, na vilevile mashauriano na wadau wengine ikiwemo Mamlaka ya Kitaifa ya Kukabili Dawa za Kulevya (Nacada).

Kwenye Sheria ya Fedha ya Kaunti ya 2024, Mombasa ilipandisha ada za usafirishaji wa miraa na muguka kutoka Sh24,000 hadi Sh80,000 kwa kila tani saba.