Michezo

KUFA KUPONA: Manchester United yahitaji muujiza kulaza FC Barcelona katika marudiano

April 16th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

MANCHESTER United wanahitaji muujiza mwingine hii leo Jumanne uwanjani Camp Nou, Uhispania ili kuwakomoa Barcelona na kufuzu kwa hatua ya nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

Kwingineko, Juventus watakuwa wenyeji wa Ajax kutoka Uholanzi.

Vikosi hivi viliambulia sare ya 1-1 katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliowakutanisha jijini Amsterdam, Uholanzi wiki jana.

Mshindi atakutana na ama Manchester City au Tottenham Hotspur.

Atakayetawala mchuano kati ya Barcelona na Man-United atajikatia tiketi ya kuvaana na ama Liverpool au FC Porto ya Ureno kwenye nusu-fainali.

Katika mojawapo ya mechi zao za kufuzu kwa robo-fainali, Man-United walihitaji muujiza uliowachochea kuwachabanga Paris Saint-Germain (PSG) ugenini na hatimaye kuwabandua kwenye hatua ya 16-bora kwa jumla ya mabao 3-1.

Awali, PSG walikuwa wamesajili ushindi wa 2-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliowakutanisha na Man-United uwanjani Old Trafford. Baada ya kupoteza mchuano wa mkondo wa kwanza wa robo-fainali dhidi ya Barcelona waliowapepeta 1-0 wiki jana uwanjani Old Trafford, vijana wa kocha Ole Gunnar Solskjaer kwa sasa wana mlima mrefu wa kukwea kadri wanavyopania kupiga hatua kwenye kampeni za msimu huu.

Safari ya Man-United ya kuelekea uwanjani Camp Nou inajiri takriban miaka 20 tangu Solskjaer awafungie bao la ushindi katika fainali ya UEFA iliyowakutanisha na Bayern Munich.

Solskjaer aliwatikisa nyavu za miamba hao wa soka ya Ujerumani mwishoni mwa kipindi cha pili mnamo 1999.

Tofauti na Man-United, Barcelona wanashuka dimbani kwa ajili ya mchuano wa leo wakipania kujinyanyua baada ya kulazimishiwa sare ya 1-1 na Huesca katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Mbali na Messi, Barcelona wanatarajiwa pia kutegemea ukubwa wa maarifa ya chipukizi Ousmane Dembele aliyewatambisha waajiri wake pakubwa mwishoni mwa wiki jana.

Chini ya kocha Ernesto Valverde, Barcelona waliwapumzisha masogora Messi, Philippe Coutinho, Nelson Semedo, Clement Lenglet, Sergio Busquets, Gerard Pique, Jordi Alba na Luis Suarez mwishoni mwa wiki jana kwa nia ya kuwawajibishwa vilivyo hii leo dhidi ya Man-United.

Luke Shaw nje

Man-United watalazimika kukosa huduma za beki Luke Shaw aliyepigwa marufuku katika mechi ya mkondo wa kwanza. Ni tukio ambalo kwa sasa linamsaza kocha Solskjaer katika ulazima wa kutegemea huduma za beki Ashley Young kwenye safu ya ulinzi.

Ingawa Solskjaer huenda akalazimika kudumisha kikosi alichokitegemea dhidi ya PSG.

Hata hivyo, mfumo wa kumwajibisha Jesse Lingard kama mfumaji mkuu akisaidiwa na Romelu Lukaku na Marcus Rashford huenda ukawasaidia Man-United kuwabwaga wenyeji wao kirahisi.

Ingawa Barcelona hawakudhihirisha ubabe wao uwanjani Old Trafford, huenda wakapata fursa ya kutamba zaidi dhidi ya wenyeji wao katika mchuano wa leo kwa matarajio kwamba watachuma nafuu zaidi kutokana na wingi wa mashabiki wao wa nyumbani.

Dhidi ya timu bunifu na yenye makali kuliko United, Barcelona ilibahatika kutoadhibiwa kwa mchezo duni usioisawiri kama timu inayofaa kuorodheshwa kama mgombeaji halisi wa taji la UEFA msimu huu.

Barcelona mara nyingi walikosa udhibiti, lakini wakaponyoka na ushindi muhimu ulioonyesha kukosekana kwa makali katika safu ya mashambulizi ya Man-United kama tu ile ya wageni wao.

Mchezo duni uliojaa pasi mbovu na mchango mdogo wa kushangaza kutoka kwa Messi ulizalisha si tu ushindi, bali goli muhimu la ugenini walilorejea nalo nyumbani uwanjani Camp Nou, Uhispania.