Michezo

Kufa kupona: Mikel kuchezeshwa akiwa na jeraha dhidi ya Argentina

June 25th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

NAHODHA wa Nigeria, John Obi Mikel anatarajiwa kucheza mechi ya Argentina hapo Jumanne akivalia plasta baada ya kujeruhiwa mkono katika mechi ya Iceland ambayo Super Eagles ilishinda 2-0 Juni 22, 2018.

Taarifa kutoka nchini Nigeria zinasema kwamba Mikel alitoka uwanjani kwa muda mfupi akiwa na uchungu katika dakika za lala-salama, lakini alilazimika kuendelea na mechi kwa sababu kocha Gernot Rohr alikuwa ameshafanya mabadiliko yote matatu.

Mnamo Juni 23, Mjerumani Rohr aliambia runinga ya KweseESPN kwamba jeraha hilo si baya na kwamba Mikel atashiriki mchuano wa Argentina. Alipeana mwangaza tena kuhusu jeraha la Mikel hapo Juni 24 akisema, “Kwa bahati mbaya, kuna jeraha moja. Nahodha ana jeraha la mkono (mifupa ya kiganja), lakini nadhani anaweza kucheza akivalia plasta.

“Kikosi chetu cha madaktari kinamshughulikia,” Rohr alisema kupitia video iliyochapishwa katika mtandao wa Twitter wa Super Eagles.

Nigeria ilifunga safari ya kuelekea mji wa Saint Petersburg siku ya Jumapili ambako itakabiliana na Argentina hapo Juni 26 katika mechi itakayoamua nani kati yao ataingia raundi ya 16-bora.

Croatia inaongoza Kundi D kwa alama sita, mbili mbele ya nambari mbili Nigeria nazo Iceland na Argentina zina alama moja kila mmoja.