Habari

KUFA KUPONA: Tanzania nayo yajipa tumaini mechi dhidi ya Kenya

June 27th, 2019 3 min read

Na IMANI MAKONGORO

CAIRO, MISRI

KENYA ina fursa nzuri ya kujinyanyua leo Alhamisi kwenye kampeni za AFCON kwa kuchabanga majirani zao Tanzania ambao pia walipoteza mchuano wao wa ufunguzi wa Kundi C dhidi ya Senegal mwishoni mwa wiki jana.

Ushindi kwa Kenya ambao wataenedelea kuzikosa huduma za beki Joash Onyango wa Gor Mahia, utaweka hai matumaini yao ya kusonga mbele katika kampeni za mwaka huu iwapo Senegal watakizamisha chombo cha wapinzani wao Algeria katika mechi nyingine ya leo.

Hali hii itawaweka katika ulazima wa kuwapepeta Senegal katika mchuano wao wa mwisho wa makundi hapo Julai 1 kwa matarajio kwamba Tanzania nao watawabana au kuwazidi maarifa Algeria katika kibarua cha funga-kazi kwenye Kundi C.

Onyango alipata jeraha la kifundo cha mguu saa chache kabla ya Kenya kuchuana na Algeria. Awali, Kenya ililazimika kupoteza huduma za beki Brian Mandela aliyeumia katika kambi ya mazoezi jijini Paris, Ufaransa.

Timu mbili za kwanza zitakazotawala vilele vya makundi yote sita zitatinga raundi ya 16-bora moja kwa moja, huku vikosi vinne vingine vitakavyokamilisha mechi za makundi katika nafasi za tatu kwa kujizolea alama nyingi zaidi pia vikijikatia tiketi za kunogesha awamu hiyo ya mwondoano.

Wakicheza dhidi ya Kenya katika mechi yao ya ufunguzi wa Kundi C, Algeria walifungiwa bao na Baghdad Bounedjah kupitia mkwaju wa penalti kabla ya Riyad Mahrez wa Man-City kufunga goli jingine lililowazima kabisa vijana hao wa kocha Sebastien Migne mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Jaribio la pekee la Kenya langoni pa Algeria lilikuja mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya kombora la mvamizi Michael Olunga wa Kashiwa Reysol kunyakwa na kipa Aissa Mandi aliyesalia langoni kwa muda mrefu bila ya kufanyishwa kazi yoyote na kikosi cha Kenya.

Uwepo wa kiungo na nahodha Victor Wanyama wa Tottenham Hotspur mbele ya mabeki wengi wa Kenya ni jambo linalotarajiwa kuwanyima Tanzania fursa yoyote ya kujipenyeza katika ngome ya wapinzani wao.

Katika mechi nne za kufuzu kwa fainali za AFCON mwaka huu, Kenya walifungwa mabao mawili pekee (dhidi ya Ghana na Ethiopia). Isitoshe, waliwaduwaza Ghana kwa kusajili ushindi wa 1-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliowakutanisha jijini Nairobi kabla ya wao pia kupokezwa kichapo sawa na hicho katika marudiano yaliyoandaliwa jijini Accra.

Migne ambaye alipania kuongoza Kenya kuiziba sana ngome yao dhidi ya Algeria, anatazamiwa kumtegemea tena Olunga katika safu ya mbele kwa matarajio kwamba atashirikiana vilivyo na kiungo Johanna Omollo aliyebadilisha kasi ya mchezo baada ya kutokea benchi kunako dakika ya 70 wikendi jana.

Mpango wa kusukumana

Japo mpango wa Tanzania ulikuwa wa kusukumana na kutumia nguvu nyingi zaidi dhidi ya Senegal katika mechi ya kwanza ya Kundi C, mikakati hiyo iliwaweka katika hatari ya kulishwa kadi nyingi zaidi za manjano.

Keita Balde na Krepin Diatta waliwafungia Senegal almaarufu ‘Lions of Teranga’ mabao katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Tanzania ambao watajipata wakifunganya virago mapema nchini Misri iwapo watakwaruzwa na Kenya. Tanzania ambao wanarejea katika fainali za AFCON baada ya miaka 39, walisalia kumtegemea zaidi kipa Aishi Manula aliyepangua zaidi ya fataki 20 zilizoelekezwa na Senegal langoni pake.

Mbali na umahiri wa Manula langoni, Kocha Emmanuel Amunike anatarajiwa kutegemea zaidi kipaji cha mvamizi Mbwana Samatta aliyetawazwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Ubelgiji msimu huu.

Katika kikosi anachojivunia nchini Misri, Migne ana makipa watatu, mabeki wanane, viungo tisa na mafowadi watatu. Kocha huyo aliyewahi kuwa msaidizi wa veterani Claude Leroy nchini Congo, atalenga sana kuvamia timu ya Tanzania badala ya kuzuia kama alivyoshauri vijana wake kufanya dhidi ya Algeria.

Huenda pia akampanga Paul Were katika kikosi cha kwanza kwa nia ya kuwapiga jeki Johanna na Ayub Timbe – wachezaji chipukizi ambao wana nguvu ya kuwania mpira kutoka kwa wapinzani, kupiga chenga na kushambulia kwa kushtukiza. Kasi yao itawasaidia kumpokeza Olunga pasi nyingi kwa urahisi.