NASAHA: Kufeli kunapaswa kukupa nguvu mpya badala ya kukukatiza tamaa

NASAHA: Kufeli kunapaswa kukupa nguvu mpya badala ya kukukatiza tamaa

Na HENRY MOKUA

JAMII imetuzoesha kuukubali ushindi daima na kuchukia kufeli.

Stadi zinazoangaziwa mno ni za kuyasherehekea matokeo bora.

Tunachelea hata kuwafunza watoto wetu kwamba maisha ni kama sarafu iliyo na pande mbili na daima hazitenganishwi; yaani, lazima uwe unaitazama mojawapo kwa wakati mmoja.

Yamkini, hali hii ndiyo imechangia visa vingi vya kujitoa uhai na hata kuwaangamiza wengine wanapoyakiuka matarajio yetu.

Suala la matazamio (expectations) linazidi kuzua mjadala miongoni mwa makundi mbalimbali ya jamii. Nimelishudia hili kwa mara nyingine majuma machache yaliyopita.

Wafanyakazi wa kampuni fulani walipelekwa kwenye ziara. Sehemu zote walizozuru, mahali walipolala na vyakula walivyovila vyote viliungana kuipamba ziara ile ikawa ya kuvutia kweli. Jambo moja lakini liliitia ziara ile dosari — masurufu waliyopewa yalikuwa ya kukatiza tamaa.

Iweje kiasi kikubwa tu cha hela kitumiwe kununulia chakula, kulipia mahali pazuri pa kulala na pa kuzuru kisha tupewe masurufu ya kutamausha kiasi hiki? Walijiuliza.

Waliwahi kulalamika mno hadi taarifa zikamfikia mkuu wao. Ajabu hata hivyo ni kwamba walikumbuka kumshukuru mkuu baada ya malalamishi kumfikia. Walikiri baadaye kwamba waliifurahia ziara yenyewe na suala la masurufu ndilo tu halikuwapendeza!

Je, ewe mwanafunzi, matazamio yako binafsi ni yapi?

Itakapotokea kwamba hujayafikilia unawazia kuichukua hatua gani?

Utajisamehe na kujitathmini kabla ya kuyapangua na kuyapanga upya?

Je matazamio yako kwa mzazi wako ni ya kihalisia ama yanakiuka mipaka ya uwezo wake?

Kuna haja ya kuanza kuuwazia mkondo mpya; mkondo ambao utakuruhusu kukubali kufeli inapotokea kwamba umefeli. Nisije nikaeleweka visivyo — kuna kupangia kufeli na kukubali kufeli, nazungumzia kukubali. Asitokee mtu akashtakia kwamba namhimiza yeyote apangie kufeli.

Kufeli

Katika kukubali kufeli hujiwazii kwamba umeshindwa, badala yake unajipa fursa ya kuiangalia mikakati yako upya na kuamua ni wapi haikukufaa.

Hili waweza kulifanya hatua kwa hatua na hatimaye utagundua kwamba labda ulikosea mahali padogo tu pakakugharimu matokeo mazuri uliyoyatarajia.

Kama ilivyo katika michezo mbalimbali ambapo mapumziko ni muhimu, pana haja ya kukuona kufeli kama pumziko la kuyapangia upya yanayostahili kupangiwa.

Tunashuhudia mara si haba katika mchezo wa kandanda kwamba baada ya mapumziko ya mwishoni mwa kipindi cha kwanza huwapo mwamko mkubwa na nguvu mpya inayojitokeza.

Wakati mwingine timu iliyokuwa nyuma hujizoazoa na kuibuka na ushindi. Nawe wapaswa kukuchukulia kutoyafikilia malengo yako kama fursa ya kuitwaa nguvu mpya na kuyawania matazamio yako hayo kwa mara nyingine.

Wakati ukifanya vile, wazia pia kwamba matazamio yako kwa mzazi au mwangalizi wako yatakuathiri kwa namna fulani. Yatathmini vilivyo kabla ya kuafikiana na nafsi yako kwamba yanastahiki. Yakiwa juu mno, labda kutokana na kumlinganisha na wazazi wa wenzio huenda ukajikuta katika msongo wa mawazo.

Msongo huu utakusababisha kushindwa kuyaelekeza makini yako kwenye masomo yako kikamilifu. Hatima ya hali hii ni kukosa kuyafikilia malengo yako bila shaka.

Matazamio yako kwa mwalimu wako ni ya umuhimu mkubwa hali kadhalika. Ikiwa huna hakika kuyahusu matazamio yako kwake wazia kushauriana naye ili muufikie mwafaka kulihusu jambo hili.

Siri ni hii: jiwekee matazamio ya kufikilika! Mwekee mzazi na mwalimu wako matazamio ya kufikilika hali kadhalika. Ukifanya hivi kufeli kukatokea itathmini mikakati yako upya na ujitose tena ukiwa na nguvu mpya, hatimaye mambo yatatengenea tu!

You can share this post!

Mke asukumia mume mhanyaji kipusa

Messi afunga mabao mawili na kusaidia PSG kutoka nyuma na...

T L