Kimataifa

Kufunga kula kwaweza kuponya saratani – Utafiti

July 24th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

WANASAYANSI wamegundua kuwa kufunga kula kunasaidia mwili kuboresha kinga dhidi ya magonjwa, kwa kuzipa nguvu chembechembe ambazo hupigana na maumivu.

Katika jarida lililochapishwa na watafiti kutoka chuo kikuu cha Southern California, wanasayansi hao walibaini kuwa mtu anapofunga kula, hali hiyo huamsha seli za mwili kwa jina ‘Stem Cells’, zinazofanya kazi kama askari kupigana na magonjwa

Waligundua kuwa mtu anapofunga, seli hizo ikiwa zilikuwa zimelala huwa zinaamka na kuanza kufanya kazi, kwa kupata nguvu mpya.

Utafiti huo ulifanywa kwa wagonjwa wa Saratani ambao walikuwa wakipokea matibabu, ambao walikaa kwa muda mrefu bila kula.

“Hatukutarajia kuwa kufunga kwa muda mrefu kunaweza kuwa na matokeo mazuri hivyo, kwa kufufua seli hizo. Mtu anapopatwa na njaa, mwili unajaribu kuokoa nguvu na mbinu moja ni kwa kuamsha seli ambazo zilikuwa zimekosa kazi, ama zilizokuwa zimejeruhiwa,” akasema Valter Longo, mmoja wa watafiti hao.

Watafiti hao aidha walisema kuwa kufunga husaidia kupunguza chembechembe za PKA enzyme ambazo zimehusishwa na kuleta uzee na saratani.

Aidha, watafiti hao walisema kwa wagonjwa wa saratani, kufunga kabla ya matibabu ya Chemotherapy husaidia kupunguza majeraha kwa viungo vya mwili.

“Chemotherapy husababisha majeraha kwa kinga za mwili, lakini mtu akifunga kabla ya kufanyiwa yanapungua,” akasema Tanya Dorff, mtafiti mwingine.

Jamii nyingi zimekua zikiendeleza utamaduni wa kufunga, kwa sababu tofauti.

Wanasayansi wengine waligundua kuwa kufunga kuna uwezo wa kuzuia magonjwa ya akili, moyo, sukari na pia kuponya saratani.