Kufungwa kwa hoteli ya kihistoria pigo kwa maskauti

Kufungwa kwa hoteli ya kihistoria pigo kwa maskauti

Na MERCY MWENDE

KUFUNGWA kwa hoteli ya kihistoria ya Outspan, alimoishi mwanzilishi wa maskauti duniani Lord Baden Powell kumekuwa pigo kuu kwa maadhimishio ya Siku ya Founderee’s mjini Nyeri, Jumamosi.

Akisema kwa njia ya kipekee na Taifa Leo Dijitali, meneja wa hoteli hiyo Bw Christopher Atheka alisema biashara hiyo ilifungwa Aprili, 2020 baada ya kukosa mapato kutokana na vizuizi vya usafiri vilivyoletwa na janga la Covid-19 vilivyowekwa na serikali.

Meneja huyo alieleza kuwa hoteli hiyo huwategemea watalii wa nje, lakini mwaka huu, tofauti na hapo mbeleni, maskauti waliruhusiwa tu kufanya gwaride mbele ya lango la hoteli kabla ya kuandamana katika makaburi ya St Peter alimozikwa Bw Powell na mkewe Bi Olave Powell.

“Biashara hii, haswa hutegemea wateja wa kulala na hivyo bado hatujawapata wateja tosha watakaotuwezesha tuifungue tena hoteli kuisherehekea hafla hii,” akasema Bw Atheka.

Imebainika kuwa hoteli hiyo inayosimamiwa na Bodi ya Aberdare Safari Limited imo hatarini kuwekwa mnadani kwa kukosa hela, huku Bw Atheka akisema bado wako katika harakati za kuifungua tena.

Katika jengo la Paxtu lililo katika hoteli hiyo, kipo chumba cha kulala alimoishi Bw Powell na mkewe kutoka mwaka wa 1939 hadi Januari 8, 1941 alipofariki.

Pamehifadhiwa pia, samani alizotengeneza na kuzitumia wakati huo. Katika hafla za awali, maskauti kutoka mataifa tofauti duniani waliruhusiwa kukitembelea chumba hicho ambapo walifunzwa kuyahusu maisha ya Bw Powell na bibiye.

Pia, walikuwa wakipiga kambi katika hoteli hiyo kwa muda wa siku nne kabla ya kuiadhimisha sherehe hiyo.

Kulingana na Afisa Mkuu wa Shirika la Maskauti Nchini (KSA) Moses Danda, katika hafla ya mwaka huu wamepunguza idadi ya maskauti watakaoihudhuria kutoka 2,000 mwaka wa 2019 hadi 100.

Katika maadhimisho ya mwaka 2019, waliwaalika maskauti hasa wenye umri wa miaka kati ya 12 hadi 18 ingawa wakati huu waliwachagua tu maskauti wa vyuo vikuu wenye cheo cha Rovers.

“Hatukutaka kuiingilia ratiba ya maskauti walio katika shule za msingi na sekondari kwani tayari janga la Covid-19 lilikuwa limekatiza masomo yao,” alileza Bw Danda.

Aliwaagiza walimu waziandae hafla zao wenyewe shuleni ili maskauti waweze kuiadhimisha siku hiyo.

Maskauti wa vyeo vya Rovers katika kaunti mbalimbali pia waliombwa wajishughulishe katika miradi ya kuisaidia jamii watakapokuwa wakiiadhimisha sherehe hiyo.

Kulingana na historia, baada ya kifo cha Bw Powell, Bi Olave alirudi nchini Uingereza alipoishi hadi mwaka wa 1977 alipofariki.

Ingawa baadaye, mwili wake ulisafirishwa na mjukuu wake na akazikwa kando ya mumewe katika makaburi ya St Peter mjini Nyeri.

  • Tags

You can share this post!

BBI: Magari kwa madiwani, wilbaro kwa vijana

Ugonjwa usiojulikana wafyeka kondoo 2,000 Gilgil