Kufutwa kazi Kulundu kwakera Azimio

Kufutwa kazi Kulundu kwakera Azimio

NA CHARLES WASONGA

WABUNGE wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya wamemtaka Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati abatilishe hatua ya kumfuta kazi Naibu Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Ruth Kulundu.

Wakiongozwa na kiongozi wa Wengi Opiyo Wandayi, wabunge hao 20 wamempa Bw Chebukati makataa ya saa 48 kufutilia mbali hatua hiyo la sivyo wachukue “hatua kali”.

Wakiongea na wanahabari Jumatano katika mkahawa wa Safari Park, Nairobi, wabunge ha walidai Bi Kulundu alifutwa kazi kinyume cha sheria na kwa msukumo wa kisiasa.

“Leo Naibu Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC Bi Ruth Kulundu amefutwa kazi na makamishna watatu wa IEBC wakiongozwa na Chebukati. Tungependa kusema hapa kwamba kitendo hicho ni haramu kwani kimechochewa na matukio ya kura za urais katika ukumbi wa Bomas of Kenya,” akasema Bw Wandayi ambaye ni mbunge wa Ugunja.

Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi na wabunge wenzake wakilaani hatua IEBC kumfuta kazi naibu afisa mkuu mtendaji wa IEBC Ruth Kulundu. Hapa ni hoteli ya Safari Park jijini Nairobi. PICHA | CHARLES WASONGA

Mbunge huyo, aliyekuwa ameandamana na wenzake, alisema hatua kama hiyo haiwezi kuchukuliwa na makamishna watatu pekee bila wenzao wanne kushirikishwa.

“IEBC sio makamishna wawili pamoja na Chebukati. Hawawezi kujitwika mamlaka ya kumfuta kazi afisa wa cheo cha juu kama naibu afisa mkuu,” Bw Wandayi akaongeza.

Kwa upande wake, Mbunge Maalum Sabina Chege alitaja kufutwa kazi kwa Bi Kulundu kama dhuluma dhidi ya wanawake.

“Kama mbunge maalam aliyeteuliwa kuwakilisha wanawake, nashutumu vikali kufutwa kazi kwa Bi Kulundu. Tunajua kuwa afisa huyo ameadhibiwa kwa kufanya kazi yake ipasavyo wakati wa uchaguzi. Kufanya kazi kwa njia inayofaa sio kosa na tunampa Chebukati makataa ya saa 48 amrejeshe kazini la sivyo tutachukua hatua kali dhidi ya tume hiyo,” akafoka.

 

Mbunge Maalum Sabina Chege akilaani kupigwa kalamu kwa Naibu Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Ruth Kulundu. PICHA | CHARLES WASONGA
Mbunge Mwakilishi wa Kike Nairobi Bi Sabina Chege akilaani kupigwa kalamu kwa Naibu Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Ruth Kulundu. PICHA | CHARLES WASONGA

Duru zilisema kuwa Bi Kulundu aliadhibiwa kwa kuunga mkono makamishna wanne waliokataa ushindi wa Rais William Ruto kulingana na matokeo yaliyotangazwa na Bw Chebukati Bomas, Agosti 15.

Makamishna hao ni; Naibu Mwenyekiti Juliana Cherera, Francis Wanderi, Justus Nyang’aya na Irene Masit.

Hata hivyo, wanne hao walibadili msimamo wao na kuunga mkono ushindi wa Dkt Ruto baada ya kuidhinishwa na Mahakama ya Upeo mnamo Septemba 5, 2022.

Wabunge wa Azimio wanasema Chebukati na makamishna Abdi Guliye na Boya Molu hawafai “kujitwika mamlaka ya kumfuta kazi Bi Kulundu ilhali muda wao wa kuhudumu unaisha Januari 2023.”

“Watatu hawa wanafaa kwenda likizo ya mwisho kabla ya kwenda nyumbani. Wakome kuwadhulumu maafisa wa tume hii,” akasema Mbunge wa Navakholo Emmanuel Wangwe.

  • Tags

You can share this post!

Wafugaji walia chagamoto kibao zimezingira biashara ya kuku

TAHARIRI: Njia za kujiondoa kutoka muungano wa kisiasa zi...

T L