HabariSiasa

Kujiuzulu kwa Chebukati kutampa mwanya Chiloba kurejea IEBC – John Mbadi

April 18th, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa wachache katika Bunge la Kitaifa John Mbadi Jumatano amepinga shinikizo za kumtaka mwenyekiti wa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati na makamishna wawili wang’atuke haraka. 

Akiongea wa wanahabari Jumatano afisini mwake katika majengo ya bunge, Bw Mbadi alisema Bw Chebukati na makamishna Profesa Abdi Guliye na Boya Molu wanafaa kuendelea kushikilia nyadhifa zao ili kutoa nafasi kwa “Wakenya kukubaliana kuhusu njia mwafaka za kuifanyia tume hiyo mageuzi kamili”

“Natofautiana kabisa na kauli za wenzangu, Aden Duale, Kipchumba Murkomen na James Orengo kwamba Chebukati na wenzake wajiuzulu.

Hatua hiyo itatoa nafasi kwa Chiloba kurejea katika jumba la Anniversary na kuendelea kuharibu mambo kule,” akasema.

Mbandi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini alipendekeza kwa mageuzi katika IEBC yaanza katika sekritariati ya tume hiyo inayoongozwa na Bw Chiloba ambaye amepewa likizo ya lazima ya miezi mitatu kutoa nafasi kwa uchunguzi kuhusu sakata ya ufisadi.

“Chiloba na maafisa wote katika sekritariati ya IEBC ndio wanafaa kuondolewa kwanza kabla ya Chebukati na wenzake. Chimbuko la matatizo yanayoizonga tume hii ni Chiloba,” akasema Bw Mbadi.

Alidai Mbw Duale na Murkomen wanataka Chebukati na wenzake waondoke haraka ili kutoa nafasi kwa “Bw Chiloba kurejea katika IEBC ili kuweka mikakati ya wizi wa kura katika uchaguzi mkuu wa 2022.

“Sisi kama NASA hatutakubali Chiloba kuendelea kushikilia wadhifa huo. Anafaa kufutwa kazi na kisha kufunguliwa mashtaka kortini,” akasema.

Bw Chebukati alikuwa amepuuzilia mbali wito wa kumtaka ajiuzulu na badala yake akasema inafaa wabunge waweke mikakati ya kupitisha sheria itakayotoa mwongozo wa jinsi ya kuajiri makamishna watakaojaza nafasi zilizoachwa wazi.

“Bunge halijapitisha sheria ya kusimamia jinsi ya kuajiri makamishna kuchukua mahala pa wale wanaoondoka. Hivyo basi, tunaomba asasi husika za serikali zichukue hatua zinazofaa ili kuhakikisha majukumu ya tume hayakwami,” akasema.

Kulingana naye, makamishna Consolata Nkatha Maina (Naibu Mwenyekiti), Dkt Paul Kibiwott Kurgat na Margaret Wanjala Mwachanya ambao walijiuzulu walionyesha hawana uwezo wa kuongoza tume inapokumbwa na matatizo, na pia si wenye moyo wa kukumbatia maoni yanayotofautiana na misimamo yao.