Habari Mseto

Kukamilika kwa mwezi Mtukufu wa Ramadhani kusiwe mwisho wa ibada

April 10th, 2024 1 min read

NA JUMA NAMLOLA

KWANZA hatuna budi kurejesha shukurani kwa Mwenyezi Mungu (SWT) kwa kutupa nafasi ya kushiriki katika ibada kubwa ya kufunga. Hii ni nguzo ya nne ya Uislamu.

Hatimaye Ramadhani imekamilika. Ni mwezi uliokuwa na malipo mengi. Waumini walijizuia; kusengenya, kutukana, kuteta, kupigana, na kusema uongo kati ya maovu ya kijamii.

Kulikuwa na usiku wa Laylatul-Qadir ambao ubora wake ni sawa na miezi 1,000 au miaka 83 na nusu. Huenda baadhi ya waliosimama usiku katika siku kumi za mwisho, walibahatika kuupata usiku huo.

Punde tu baada ya kusherehekea sikukuu ya Idd-Ul-Fitri, kuna sunnah ya kufunga siku sita.Kulingana na mtume (SAW), “Yeyote mwenye kufunga mwezi wa Ramadhani, na kuufuatiliza na siku sita za mwezi wa Shawwal, atakuwa malipo yake ni sawa na mtu aliyefunga kwa mwaka mzima.”

Kukamilika kwa Ramadhani kusiwe ni mwisho wa ibada. Kuna wengi walioacha anasa, mambo ya kipuzi na kujazana misikitini wakiswali na kusoma Kur’ani. Mambo haya yanastahili kuendelezwa hata baada ya Ramadhani.

Hatimaye naushukuru usimamizi wa Nation Media Group kwa fursa ya ukumbi huu. Napaswa kuwatambua Mhariri Msimamizi Bw Gilbert Mogire, wahariri Sylvester Mukele, Lucy Kilalo, Ali Abubakar, Stephen Musamali na Fatuma Bariki. Kuna Bi Alice Othieno aliyesarifu kurasa na ndugu Benson Matheka aliyeondoa mategu.

Nawatambua pia ndugu Khamis Mohamed na Ali Hassan waliotenga muda wakati wa ibada zao, kutuandalia Makala ya Nasaha za Ramadhani.

Lakini shukurani zangu za dhati ni kwako msomaji. Bila wewe, ukurasa huu haungekuwapo.

Tunakuombea uzima na uwezo wa kuendelea kusoma magazeti yetu ya Taifa leo, Taifa Jumapili na wavuti wetu wa www.taifaleo.nation.co.ke.