Bambika

Kukosa meneja sababu yangu kuanguka jukwaani – Stivo Simple Boy

March 16th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

RAPA Stephen Otieno almaarufu Stivo Simple Boy, amesema kuondoka kwa meneja wake ndio sababu ya yeye kuanguka wakati wa kipindi cha burudani cha ‘10 Over 10’ kinachopeperushwa na runinga ya Citizen.

Mwanamuziki huyo alianguka mnamo Ijumaa.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo mnamo Jumamosi, alisema meneja wake aliondoka majuzi, hali ambayo “huniletea mawazo mengi”.

“Kwa sasa niko sawa. Lakini huwa naishiwa na nguvu kwa kumkosa meneja wangu. Kuna watu walio na nia ya kutukosanisha,” alisema Stivo Simple Boy.

Aliongeza kwamba kukosa meneja kunafanya anakuwa na ‘stress’ hadi inafika wakati akiwa jukwaani, anaanguka bila kutarajia.

“Ukiwa mwanamuziki tajika, huwezi ukafanya kazi bila meneja,” akaeleza.

Stivo Simple Boy akizungumza na mtangazaji nahodha wa kipindi hicho ’10 Over 10’ Azeezah Hashim, alidondoka na kuanguka ghafla.

Hali hiyo ilisababisha mabadiliko kwa dakika kadhaa, huku onyesho hilo likisitishwa kwa muda ili kuhakikisha kuwa mwanamuziki huyo anashughulikiwa.

Baada ya muda mfupi, habari ziliibuka kuwa alikuwa amerejewa na fahamu na alikuwa yuko katika hali nzuri.

Mtangazaji wa kipindi alimtafuta kwa njia ya simu ambapo msanii huyo anayetambulika kwa ‘Ndio Manake’ alimhakikishia yeye na mashabiki wake waliokuwa na wasiwasi kuwa alikuwa anaendelea vyema.

“Niko sawa na hivi karibuni nitarudi,” alisema.

Stivo alianguka alipokuwa akizungumzia uzoefu wake na jinsi maisha yalivyokuwa akilelewa katika mtaa duni wa Kibera na pia umaarufu wake nyumbani kwao Ugunja, Kaunti ya Siaya.

Mwanadensi mmoja wa kike ambaye alikuwa ametoka kwa shoo hiyo ya ’10 Over 10’ alisimulia tukio hilo la Stivo kuanguka akisema “tulienjoi shoo lakini tulishtuka msanii huyo alipoanguka ghafla”.