Siasa

‘Kulala njaa Mlima Kenya ni kujitakia’

June 5th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

SIASA za mipasuko ambazo zimenoga kwa sasa katika ukanda wa Mlima Kenya, zimegeuka kuwa mifereji ya pesa kwa wenyeji ambapo baadhi wanaomba zidumu.

Mirengo ya kukodisha huduma ambayo imezuka imekuwa afueni kuu kwa baadhi ya wenyeji ambao wanajua ‘kukulia siasa’.

Kwa sasa, mirengo ambayo imezuka ni ile inayosemwa kuongozwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua, mbunge wa Kiharu Bw Ndindi Nyoro, Gavana wa Kirinyaga Bi Anne Waiguru, mbunge wa Laikipia Mashariki Bw Mwangi Kiunjuri na pia wengine wakiwa kwa mrengo wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na wa Rais wa Tano Dkt William Ruto.

Siasa hizo hata zinasemwa kwamba zimechochewa kimakusudi na madalali wa makabiliano ambao huwa weledi wa kuzua na kuendeleza mipasuko ili kujiundia nafasi za kuchuma riziki.

Baadhi ya wanaokula vinono kutokana na mipasuko hiyo ni pamoja na viongozi waliochaguliwa ambao wanachumbiwa kujiunga na mirengo hiyo ili kuiimarisha na kuipa makali, viongozi wa kijamii, wachungaji ambao hutoa nafasi kwa wanasiasa wahutubie washirika, wazee na pia makundi ya mashinani.

“Ili kujitokeza katika mkutano wa mrengo fulani, ni lazima ulipe gharama ya Sh500 kwa kila shabiki wa kukodishwa. Madalali wa kushirikisha ushabiki huo hulipwa Sh1,000 kwa kila mmoja lakini wakiishia ‘kuwaibia’ mashabiki kwa kuwalipa Sh200 kila mmoja badala ya zile Sh500 zilizo kwa bajeti,” asema mshirikishi wa masuala ya vijana ukanda wa Mlima Kenya Bw Warui Gitau.

Hata waandishi wa habari hawajaachwa nyuma ambapo baadhi wanasakwa ili kusaidia kulipa mirengo hiyo vichwa vya habari kwa ‘shukran’ ya kitu kidogo.

“Mimi nimepata simu kadha za kunichumbia nisaidie mirengo kadha na mawazo ya kugonga vichwa vya habari. Wengine wanataka stori zao zitokee kwa masharti yao wakiahidi kulipa vizuri. Ni siasa ambazo ziko na majaribu mengi sana ya kitaaluma,” asema mwandishi mmoja wa habari.

Wengine, miongoni mwao madereva wa teksi katika mji wa Murang’a, wanafichua kwamba mwanasiasa mmoja wa kaunti hiyo amekuwa akikutana na madiwani wa kaunti nyingine katika afisi yake Jijini Nairobi.

“Ili kukwepa kujulikana na kutambuliwa kwa njama anayosuka, amekuwa akiwapa kazi madereva wa teksi ambao anaweza akawaamini,” asema mhudumu mmoja wa teksi.

Mhudumu huyo anafichua kwamba mwanasiasa huyo hujaribu kila awezalo kuhakikisha madiwani lengwa hawatumii magari yao.

“Kinachofanyika ni mhudumu wa teksi kupigiwa simu na wasaidizi wa mwanasiasa huyo na kuagizwa afike katika kaunti fulani kuchukua diwani mmoja au madiwani kadhaa na uwafikishe Nairobi,” asema.

Anaongeza kwamba “unaweza ukatumwa hadi kaunti za Nakuru, Nyandarua, Laikipia, Meru, Tharaka Nithi, Kirinyaga na Embu ambako siasa hizo zimeshika kasi”.

Patroni wa Baraza la Wazee wa Mlima Kenya Bw Kung’u Muigai anasema kwamba kuna baadhi ya mirengo ya wazee ambayo imezuka ya kuuza baraka kwa wanasiasa.

“Kuna wazee wetu hapa kwa Mlima ambao wanapanga hafla bandia za kuwabariki wanasiasa na kuwateua kuwa wazee wa kijamii pasipo kufuata utaratibu uliowekwa wa kitamaduni,” asema Bw Muigai.

Bw Muigai anasema kwamba “hii ni hali ya kawaida ambayo huzuka kila mara kukiwa na ushindani wa kisiasa”.

Anasema kwamba hali hiyo ndio imefanya siasa za Mlima Kenya kuwa na mirengo kwa kuwa kuna wale watazidi kufanya juu chini ndio kuwe na farakano ili mianya ya riziki idumu.

Bw Muigai anasema “hata nikiwa mwandani wa serikali hii, ninaweza nikakufichulia kwamba haya makongamano unasikia ya Limuru huwa yamechochewa na mirengo ili wanasiasa fulani watoe ufadhili”.

Kulikuwa na kongamano la Limuru III mnamo Mei 2, 2024, ambalo inadaiwa halikuacha Sh20 milioni zikiwa na chenji.

Mabaunsa nao wamekuwa katika soko huku wakikodishwa kuandamana na wanasiasa na pia kuwafanyia kazi za kushirikisha magenge ya kushangilia na ikibidi, kukabiliana.

Mbunge wa Thika Mjini Bi Alice Ng’ang’a anasema kwamba “siasa za kaunti ndizo hatari zaidi kwa kuwa magenge na mabaunsa wa kulipwa hata wanaweza wakakuua kwa malipo ya mia kadha”.

Bi Ng’ang’a alilazimika kulala ndani ya mtaro wa majitaka wakati ghasia zilizuka Kigumo.

Soma Pia: Mbunge asimulia jinsi alivyolazwa kwa mtaro kuepuka kifo

Wanamuziki na wacheshi ni wengine ambao wamekuwa katika soko la kisiasa wakivuna vilivyo katika siasa hizo za kimirengo.

Baadhi ya wasanii hao hulipwa ili waachilie ngoma na vipindi vya kusifu mirengo na pia kukejeli wanasiasa wengine.

“Hata sisi mabloga hatujaachwa nyuma. Tunalipwa ili kuwaposti wanasiasa na pia kushirikisha jinsi posti hizo zitatrendi ndio kuwe na taswira ya umaarufu,” asema Bi Lydiah Mugure kutoka Nyeri.

Wakati mwanasiasa fulani anaandaa kikao na waandishi wa habari, huwa kuna wale watu wa kumzingira huku wakipiga makofi na kutikisa vichwa kwa kukubaliana na mwanasiasa huyo hata wakati hakuna lile la maana anasema.

Hizi zote ni hali ambazo zimezoeleka katika ulingo wa siasa.

[email protected]