Habari Mseto

Kulegeza masharti kutasabisha vifo vingi – Uhuru

June 6th, 2020 1 min read

NA MWANDISHI WETU

Wakenya mitandaoni wamezua hisia mseto baada ya Rais Kenyatta kudinda kuondoa marufuku ya kutoka na kuingia katika kaunti za Nairobi, Mombasa na Mandera huku akiongeza siku za kafyu kutoka 21 hadi 30.

Ingawa kafyu mpya itakuwa ikianza saa tatu usiku hadi saa kumi asubuhi, wakazi wa kaunti hizo tatu walitarajia kufunguliwa kwa vizuizi vilivyowekwa kuzuia wananchi kuingia na kutoka kiholela.

Rais alisema kuwa kulingana na takwimu za kisasa zilizofanywa na maafisa wa utafiti, kulegeza kamba  kwa asilimia 20 kutaleta maambukizi mapya 200,000 vifo 30,000 kutokana na Covid-19.

Kuzima matumaini ya wakazi wa kaunti hizo, Rais aliongeza kuwa kulegeza kamba kwa asilimia 40 kutazua maambukizi mengine 300,00 mapya na vifo 40,000.

Hata hivyo, amri ya kutoingia au kutoka mitaa ya Eastleigh, jijini Nairobi na Old Town, Mombasa iliondolewa kuanzia Jumapili huku kaunti za Kilifi na Kwale zikifunguliwa.

“Hakuna jambo amefanya hapo. Kufungua Kwale na Kilifi na kufunga Mombasa hainiingii akilini. Watu watapita tu kwani wengi hufanya kazi Mombasa,” alisema Mkenya mmoja kwenye Facebook.

“Angetufungulia Nairobi tusafiri kidogo maanake tumechoka kuishi mahali pamoja,” alidakia mwingine.

Wengine walisema kuwa Tanzania haijawahi kufunga biashara wala kuweka kafyu licha ya virusi hivyo kusambaa, wakisema miili ya Watanzania itazoea ugonjwa huo na kuweza kujikinga.