Habari Mseto

Kulikuwa na tatizo la kupakia picha, Facebook yasema

March 14th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

WATUMIZI wa Facebook na Instagram walikosa huduma za mitandao hiyo ya kijamii katika maeneo tofauti ya dunia, ikiwemo Kenya Jumatano baada ya mitandao hiyo kufeli.

Kampuni hiyo ambayo ina watumizi zaidi ya bilioni mbili wa mitandao yake ilitangaza kuwa kulikuwa na matatizo ya kimitambo, wakati watumizi wa Twitter walilalamika kuwa hawangeweza kupata huduma za Facebook.

Kwa baadhi ya watumizi, japo waliweza kuingia katika mtandao wa Facebook, hawakuweza kupata baadhi ya huduma kama kutuma picha.

“Tunafahamu kuwa baadhi ya watu kwa sasa wanakumbana na tatizo la kupata huduma za Facebook na mitandao husika. Tunajaribu kusuluhisha suala hilo haraka iwezekanavyo,” ujumbe wa kampuni hiyo kupitia mtandao wa Twitter ukasema.

Muda mfupi baadaye, Facebook ilisema tatizo hili halikuhusiana kwa vyovyote na uvamizi wa kujaribu kudukua huduma zake.

“Tunathibitisha kuwa tatizo hilo halihusiani na vamizi la DDoS,” Facebook ikasema, ikipinga kile kinachosemekana kuwa kunyimwa huduma za usalama wa mitandao.

Matatizo hayo ya kukosekana kwa huduma yaliathiri zaidi Kaskazini mwa Amerika na Uropa, japo watumizi katika maeneo mengine ya dunia aidha waliathirika.

Facebook imekumbwa na matatizo sawia mbeleni, ambapo imejitetea kuwa zilikuwa shida za mawimbi na mitambo.