KUMBUKUMBU ZA SPOTI: Jagina Obore aunga mkono kuundwa timu 2 Pwani ili kurejesha heshima ya soka

KUMBUKUMBU ZA SPOTI: Jagina Obore aunga mkono kuundwa timu 2 Pwani ili kurejesha heshima ya soka

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

ALIYEKUWA mchezaji wa Black Panther FC, Mohamed Ali Obore ameunga mkono ombi lililotolewa la kutaka kuundwa timu ya Mombasa Combined kwa ajili ya kuipaisha hadi ligi kuu.

Obore amesema kunawajibika kufanyike mikakati ya kuhakikisha timu moja ama mbili zinasaidiwa ili zije kuingizwa kwenye ligi kupigania nafasi ya kupanda hadi Ligi Kuu ya Soka ya FKF.

Veterani Obore amesema anaunga mkono kwa dhati wazo hilo la kuundwa kwa timu moja ama mbili na hapo hapo zisaidiwe kwa udhamini zipate kuwa na uwezo wa kufanya vizuri na kufanikiwa kupanda ngazi hadi Ligi Kuu ya FKF.

Obore ambaye alikuwa mwanasoka wa klabu hiyo iliyoshiriki ligi kuu amesema Pwani inaweza kuunda hata timu tatu na zote zikafanya vizuri kwenye ligi kuu lakini ni sharti timu hizo zipewe udhamini kamili.

Alimsifu aliyetoa wazo hilo Mkurugenzi wa Ufundi wa Cosmos FC aliyetaka kuundwa kwa timu ya mseto ya Mombasa Combined ili kupata kurudisha heshima ya soka ya Pwani iliyokuwa nayo miaka iliyopita.

“Kwangu ningelipendelea ziundwe timu mbili moja Mombasa Combined na nyingine Coast Combined zishirikishwe kwenye Ligi ya Supa ya Kitaifa kupigania nafasi ya kupanda hadi Ligi Kuu,” akasema Obore.

Alisema jimbo la Pwani lina wachezaji wengi wazuri ambao wamesambaa kwenye klabu nyingi lakini wakiwekwa pamoja na kupata udhamini, timu za ligi kuu kutoka Pwani zitarudi kuwa nyingi.

Obore amesema ametoa wito kwa serikali za kaunti za Pwani ziitishe kikao cha washikadau wa soka pamoja wachezaji wa zamani kujadili jambo hilo ambalo anasema linastahili kuharakishwa ili timu hizo ziingizwe kwenye ligi ya msimu ujao.

Amesisitiza kuwa ana imani serikali za kaunti zitajitolea na kukubali kushirikiana kuundwa kwa timu moja ama mbili ili Pwani iweze kunawiri kama zamani nyakati katika ligi kuu kulikuwako na klabu za Mwenge, Feisal, Lake Warriors na Western Stars.

Obore amesema Mombasa Combined ambayo ilichaguliwa kutoka wachezaji wa klabu za ligi za chini za kaunti ya Mombasa, ilicheza mechi mbili ambapo ilishindwa bao 1-0 na Gor Mahia na ikafanikiwa kuishinda Bandari mabao 3-2.

You can share this post!

GUMZO LA SPOTI: Rodgers aambia Chelsea kwamba Leicester...

Ghasia zazuka Somaliland upinzani ukisisitiza kura ifanyike

T L