Makala

Kumhusu mfanyabiashara tajika wa Murang'a aliyefariki, Thayu Kamau Kabugi

February 28th, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

JUMUIYA ya wafanyabiashara nchini Kenya inaomboleza kifo cha mmoja wao, Thayu Kamau Kabugi ambaye ni mzawa wa Kaunti ya Murang’a na aliyeaga dunia wiki moja iliyopita akiwa Jijini Nairobi.

Bilionea wa uhakika kutokana na udadisi wa vigezo vya uwekezaji nchini, kabla ya kifo chake katika hospitali ya Nairobi akiwa na umri wa miaka 94 alikuwa ni mwenyekiti wa kampuni kadha; inayofahamika zaidi ikiwa ni ile ya gesi ya Astrol.

Katika salamu za pole, anaombolezwa kama mzalendo aliyethamini kuinuka kwa maisha ya wanyonge kiasi kwamba hata alikuwa akijitolea kufadhili miradi ya kimaendeleo mashinani; hasa katika kaunti ndogo ya Kiharu alikozaliwa, na Kaunti ya Murang’a kwa ujumla.

“Sijawaji kumwona mtu ambaye licha ya kula chumvi nyingi, alikuwa bado na ule uvutio wa kimawazo. Mtu ambaye katika mazungumzo yake alikuwa tu akitilia mkazo haja ya kuwapa Wakenya fursa za kimaendeleo na ajira pamoja na uwekezaji ili kuinua maisha na uchumi vilevile,” asema mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro.

Anasema kuwa alimjua Bw Kabugi miaka 20 iliyopita,  na ambapo hajawahi kuingiwa na shaka kuwa huyu mwendazake alikuwa mtu mungwana aliyewazia taifa lake na watu wote mema kimaisha na aliyekuwa tayari kujumuika na bionadamu wenzake katika mema na mabaya ya kimaisha.

Mwanglikana sugu, mwendazake aliombolezwa na Rais Uhuru Kenyatta kama aliyekuwa na ujasiri wa kipekee katika uwekezaji na ambaye mchango wake katika kupanua uchumi wa Kenya utakoswa.

“Alikuwa mzee wa hekima aliyethamini bidii ya mchwa katika maisha yake na ambaye katika hafla za kijamii, wote waliotangamana  naye watakubaliana kwamba watamkosa pakubwa,” akasema Rais katika salamu zake za rambirambi.

Aacha pengo

Rais alishabikia kampuni za mwendazake ambazo hujihusisha na masuala ya ujenzi wa nyumba za kibiashara na makazi akisema kuwa mwendazake ameacha pengo kubwa la kusaidia serikali kuafikia ajenda yake kuu kuhusu makazi.

Gavana wa Murang’a, Mwangi Wa Iria anesema kuwa marehemu Kabugi ni wa kipekee.

“Kati ya wale mabwanyenye wote ambao huhusishwa na Kauntyi ya Murang’a, ni huyu tu ambaye alikubali kushirikiana bila masharati na serikali ya Kaunti kupanua uchumi wa Murang’a,” akasema Gavana Wa Iria.

Anafichua kuwa punde tu alipochaguliwa kuwa Gavana wa kwanza wa Murang’a mwaka wa 2013, Mzee Kabugi alimwendea afisini kwa unyenyekevu na bila kutoa masharti ya kusukuma anufaike na utawala wa Kaunti, na “akakubali kushirikiana nasi katika kuhudumia watu wa Murang’a.”

Anasema huo ulikuwa ujumbe wa kipekee kutoka kwa Mzee Kabugi, ukilinganishwa na wa baadhi ya wengine ambao nia yao ya kushirikiana na utawala wa Kaunti ilikuwa wajinufaishe na kandarasi.

Hadi kifo chake, Mzee Kabugi alikuwa ndiye tu mtoto aliyesalia akiwa hai katika familia ya marehemu Kabugi Karunji na mama Grace Kabura.

Vilevile, alikuwa akiishi bila mike baada ya mauti ya kipenzi chake, Rebecca Nyambura na ambaye kwa pamoja walikuwa wamejaliwa watoto 10.

Salamu za rambirambi kutoka kwa familia yake zilimtaja mwendazake kama kiungo muhimu cha uwiano ndani ya familia yao.

Mzee huyu anarejelewa kama aliyekuwa akisaka amani idumu katika maisha yake kiasi kwamba alikuwa akihubiria familia na marafiki kuhusu busarea ya kuhepa makesi.

Pia, katika biashara, alikuwa mfuasi sugu wa itikadi kuwa ni lazima uwe mwadilifu na unapojipata katika lawama, ukubali, uombe msamaha na uridhie hasara.

Wafanyakazi katika kampuni zake wanafichua kuwa Bw Kabugi alikuwa akisisitizia wakurugenzi wake wote kuhusu busara ya kukubali makosa na kuyatafutia suluhu punde tu baada ya kugundulika yaliathiri uhusiano wao na wateja.

“Ni katika hali hiyo ambapo mwaka wa 2015 tulijipata katika kisanga cha mafuta ya petrol ambayo hayakuwa yameafikia viwango vya ubora na takriban magari 10 yaliyowekwa mafuta katika kituo chetu cha Mlolongo, yalijipata katika shida kuu ya kimitambo,” asema Bw John Mureithi, mfanyakazi na mwandani wa familia ya Mzee Kabugi.

Anasema kuwa wakati simu zilianza kupigwa katika kampuni hiyo kuhoji ni kwa nini waliuziwa mafuta yasiyokuwa yametimiza vigezo vya ubora, Mzee Kabugi aliamrisha kampuni hiyo itoe taarifa ya hadhara ya kukubali makosa, kampuni iombe msamaha na hatimaye walioathirika wapate fidia.

“Hivyo ndivyo tuliweza kujiepusha na mivutano ya mahakama. Atakayeiga busara ya mzee ataenda mabli kimaisha,” akaongeza.