Habari

Kuna chembechembe za plastiki kwa maji ya Dasani, Coca-Cola yakiri

March 16th, 2018 2 min read

Na ANNIE NJANJA

KAMPUNI ya vinywaji ya Coca-Cola imekiri uwepo wa chembechembe za plastiki katika maji ya Dasani kutokana na uchunguzi uliotolewa Alhamisi ulioonyesha kuwa brandi hiyo ni miongoni mwa asilimia 93 ya brandi za maji maarufu duniani zenye uchafu wa plastiki.

Utafiti huo unaonyesha kuwa kiwango cha uwepo wa plastiki ndani ya maji ya Dasani ni vipande 335 kwa kila lita moja ya maji hayo.

Sampuli za maji ya Dasani yaliyonunuliwa kutoka tovuti ya uuzaji bidhaa duniani ya Amazon zilikuwa na vipande vya plastiki kati ya 85 na 303 kwa kila lita.

Utafiti huo uliofanywa na wanasayansi wa Chuo Kikuu cha New York na shirika la uanahabari la Orb, ulichunguza maji kutoka Kenya, Indonesia, India, Amerika, Lebanon, Thailand, China, Mexico, Brazil na tovuti ya Amazon.

Hadi sasa, hakuna ithibati kuonyesha kuwa vipande vidogo vya plastiki ni hatari kwa afya ya binadamu.

Hata hivyo, suala hili linazidi kupata umaarufu kwa watafiti huku ongezeko la plastiki kuchafua mazingira likizidi kuwadhuru wanadamu na wanyama.

Katika mahojiano na shirika la habari la BBC, kampuni ya Coca-Cola ilisema imeweka baadhi ya viwango vya juu vya ubora kwenye sekta ya vinnywaji na soda na kuwa imekuwa ikitumia ‘mchakato wa hatua kadhaa za kusafisha maji’.

Kampuni hiyo, aidha, ilikiri kuwa vipande vidogo vya plastiki ‘hupatikana kila mahali na hivyo vinaweza kupatikana wakati wowote hata ndani ya bidhaa za maji zilizopitia mchakato wa hali ya juu wa kusafishwa.’

Watafiti hao walichunguza chupa 259 za maji zilizouzwa na brandi 11, zilizonunuliwa katika maeneo 19 tofauti katika mataifa tisa. Ni chupa 17 pekee zilipatikana bila vipande vya plastiki.

Sampuli kutoka brandi ya Nestle Pure Life kutoka Amerika zilikuwa na kiwango cha juu zaidi cha plastiki – vipande 10,390 kwa kila lita.

Uchunguzi ulionyesha kuwa vipande hivyo viliingia katika maji kwa kiwango cha chini wakati wa kuyatia chupani.

Ufichuzi huu unajiri baada ya uchunguzi mwingine kuhusu maji ya mfereji uliofanywa Septemba 2017 kuonyesha kiwango cha plastiki ndani ya maji.

“Tulipata vipande vya plastiki maradufu katika maji ya chupa kuliko maji ya mfereji kwa wastani,” ripoti ya utafiti huo ilisema.

Katika ripoti iliyochapishwa Oktoba 2017 na jarida la Uingereza la Lancet kuhusu Chembechembe za Platiki na Afya ya Binadamu, ingawa hakuna utafiti ulioonyesha kiwango cha madhara ya chembechembe za plastiki kwa afya ya binadamu, mikakati ya dharura inahitajika kupunguza uwepo wake kwa maji na kuelewa madhara ya chembechembe hizo kwa wanadamu, wanyama na mazingira kwa jumla.