Habari MsetoSiasa

Kuna mabilioni ya miradi mipya, Ruto asema

July 23rd, 2018 2 min read

Na VALENTINE OBARA

NAIBU Rais William Ruto, amepanga kuzindua miradi mipya ya mabilioni ya pesa licha ya Rais Uhuru Kenyatta kuamrisha miradi mipya isianzishwe wiki iliyopita.

Akizungumza Jumapili akiwa katika Kaunti ya Kilifi, Bw Ruto alitangaza mipango ya kuzindua ujenzi wa mabarabara na madaraja katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo katika miezi ijayo.

Miongoni mwa mipango aliyotangaza ni upanuzi wa daraja la Mtwapa ambalo limekuwa likikumbwa na misongamano ya magari kwa miaka mingi na ujenzi wa daraja Baricho.

Ingawa Bw Ruto alisema atasimamia uzinduzi wa upanuzi daraja la Mtwapa Desemba pamoja na rais, inasubiriwa kuonekana kama rais atahudhuria.

Rais Kenyatta aliagiza hakuna mradi mpya utakaozinduliwa bila idhini kutoka kwa Wizara ya Fedha hadi miradi inayoendelezwa sasa ikamilishwe ili kuzuia uharibifu wa fedha za umma.

Kulingana na naibu rais, fedha za miradi hiyo zilitengwa kwenye bajeti ya taifa na miradi mingine inafadhiliwa na pesa za mashirika kama vile Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

“Tunataka kushughulikia kila sehemu ya Kenya. Hatutaki sehemu yoyote ibaki nyuma. Tutafana haya mambo kwa sababu tunataka kuendeleza taifa mbele,” akasema.

Alikuwa akihutubu katika hafla ya kuchangisha pesa za kutafsiri Biblia kwa lugha ya Kigriama katika uwanja wa Karisa Maitha, Kaunti ya Kilifi.

Kwenye hotuba yake, Bw Ruto alionya wanasiasa dhidi ya kueneza ukabila na kugawanya wananchi.

Onyo lake lilitokea wakati ambapo wanasiasa wanazidi kujiandaa kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanywa mwaka wa 2022, ingawa kipindi cha kampeni kingali mbali mno.

USHIRIKIANO

Bw Ruto alisema wakati wa siasa ulipita na sasa inahitajika viongozi washirikiane kwa manufaa ya kuboresha maisha ya wananchi.

“Tumekamilisha mambo ya uchaguzi na vyama, sasa ni awamu ya kuhudumia wananchi. Ninawaomba viongozi wenzangu wote waliochaguliwa, nafasi tuliyo nayo sasa sio ya kuchochea matatizo bali kutafuta suluhu kwa changamoto zinazotukumba,” akasema.

Aliongeza: “Mkiona tunashirikiana hapa bila kujali vyama ni kwa sababu tumeamua hatutaki tena siasa ya kutugawanya. Hatutaki siasa ya kikabila wala kidini. Shetani tu ndiye hukasirika akiona tunafanya kazi pamoja kwa sababu yeye ndiye mkubwa wa kugawanya watu.”

Kuhusu ziara zake nyingi za eneo la Pwani, naibu rais alipuuzilia mbali wakosoaji wake na kusema hahitaji ruhusa kutoka kwa mtu yeyote kufanya ziara hizo kwani yeye ni naibu rais na ana haki ya kutembelea wananchi kusikiliza matatizo yao.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi kadhaa wa kisiasa wa Pwani wakiwemo wabunge Suleiman Dori (Msambweni), Aisha Jumwa (Malindi), Ali Mbogo (Kisauni), Owen Baya (Kilifi Kaskazini), Shariff Ali Athman (Lamu Mashariki), Badi Twalib (Jomvu), Kassim Ali Sawa (Matuga), Jones Mlolwa (Voi), Said Buya Hiribae (Galole), Benjamin Tayari (Kinango) and Paul Katana (Kaloleni).