Habari za Kitaifa

Kuna mengi hamjatueleza, wahubiri waambia Ruto na Koome

January 26th, 2024 1 min read

NA EVANS JAOLA

VIONGOZI wa kidini eneo la North Rift wanasema ni machache mno yale Rais William Ruto na Jaji Mkuu Martha Koome waliambia raia baada ya mkutano wao wa majadiliano katika Ikulu mnamo Jumatatu.

Wahubiri hao walioandaa kikao cha mashauriano mjini Kitale katika Kaunti ya Uasin Gishu, walisema ni muhimu wajue mustakabali wa nchi baada ya nguzo za urais na mahakama kurushiana cheche za maneno.

“Majadiliano baina ya nguzo kuu za serikali haiyafai kuwekwa siri. Wakenya wanasubiri kufahamu kwa kina yaliyojadiliwa na makubaliano yaliyoafikiwa, hasa kuhusu madai ya ufisadi dhidi ya Mahakama,” akasema Askofu Aggrey Olumola, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Makanisa (NCCK) tawi la Trans Nzoia.

Askofu Olumola alisikitika kwamba Rais Ruto aliibua madai kwamba mahakama inahujumu miradi ya serikali.

Wahubiri hao wameitaka ofisi ya Rais kuheshimu idara ya mahakama kama nguzo ya serikali inayojisimamia, ili itekeleze majukumu yake kwa Wakenya kwa kufuata sheria.

Askofu Olumola alishangazwa kwamba viongozi wenye doa kimaadili wanaishambulia mahakama.

Naye Mwakilishi wa Baraza Kuu la Waislamu Nchini (Supkem) Mohammed Diko alimtaka Rais Ruto kuangazia suala la ufufuaji uchumi na wala sio kuipapura mahakama.

“Rais aweke zingatio kwa ufufuaji wa uchumi na aachane na vita vya wazi dhidi ya nguzo nyingine za serikali,” akasema Bw Diko.

Serikali huwa na mihimili mikuu ambayo ni ofisi ya Rais, Idara ya Mahakama na asasi ya Bunge.

Msemaji wa Ikulu Hussein Mohammed alitoa taarifa baada ya Rais, Jaji Mkuu Koome na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula kukutana. Wengine waliohudhuria walikuwa ni Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu, na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Anne Waiguru.

Bw Mohammed alisema majadiliano yalijikita kwa mbinu za kukabiliana na ufisadi, kuimarisha uwajibikaji na kuboresha huduma kwa Wakenya.