Shangazi Akujibu

Kuna mtu ameniambia mke wangu ashamgawia bosi wake asali; roho yaniuma sana

May 15th, 2024 1 min read

Nina umri wa miaka 40 na huu ni mwaka wa 10 tangu tuoane na mke wangu. Hivi majuzi niliambiwa na mtu kwamba mke wangu ana uhusiano wa kimapenzi na bosi wake, na hata wamekula uroda. Nifanyeje?

Je, una uhakika inafanyika? Sio busara kuchukua uamuzi bila ushahidi. Fanya uchunguzi wako na ukishapata ukweli mueleze mkeo wazi. Baada ya hapo ndipo utajua uamuzi wa kuchukua.

Anataka tujaribu mbinu za kiajabu za ngono

Shangazi, katika kipindi cha hivi karibuni mke wangu amekuwa na maoni ya kustaajabisha chumbani. Juma lililopita alinifichulia kuwa anataka tuanze kujihusisha na ngono ya vikundi ili kuongeza ladha katika ndoa.

Hayo ni mageni kwangu. Sijawahi kusikia mtu akitaka kuhusisha wengine katika mahaba kwenye ndoa yake. Kumbuka pia kuna hatari za kiafya kama vile maradhi ya zinaa. Kando na hayo unaweka ndoa yako hatarini.

Jirani amekubali kunipa kila hitaji, nimkubali?

Aliponioa zaidi ya mwongo mmoja uliopita, mume wangu alikuwa akikidhi mahitaji yote ya familia yetu. Lakini sasa amepoteza ajira na kamwe hawezi kunishughulikia pamoja na wanangu kifedha. Nataka kumuacha niomoke na jirani.

Nyakati hubadilisha maishani. Unataka kumuacha eti kwa sababu sasa yupo nyakati ngumu. Je, huyo jirani akiishiwa pia utamuacha? Yote tisa, wewe pia changamka usaidia mzee kutafuta riziki ya kila siku ya familia yenu.

Ex amerudi na anataka tuwe tena wapenzi

Niko na miaka 36. Nilikuwa na mpenzi miaka kadhaa iliyopita lakini kaka huyo alinitema na kumwendea binti mwingine. Huko mambo yamechacha sasa na ananitaka tena. Nimkubali?

Huo ni uamuzi wako. Lakini jiulize ikiwa uko tayari kupitia tena machungu ya kutemwa. Henda akakufanyia vile vile kwani chui habadilishi madoa.