Habari

Kundi la wabunge lalenga kukusanya sahihi 4 milioni kuunga mswada wa BBI

November 24th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KAMATI shirikishi ya mpango wa maridhiano (BBI) imetangaza kuwa mchakato wa ukusanyaji sahihi za kuungwa mkono kura ya maamuzi utaendeshwa kwa kipindi cha wiki moja ambapo inalenga kukusanya sahihi 4 milioni.

Wenyeviti wenza wa kamati hiyo Dennis Waweru na Junet Mohammed waliwaambia wanahabari Jumatatu kwamba mchakato huo utashirikishwa na kamati mbalimbali ambazo zimebuniwa katika ngazi za kaunti zote 47.

“Ingawa, kipengele cha 257 cha Katiba kinasema kuwa mswada wa marekebisho ya Katiba kupitia kura ya maamuzi unapaswa kuungwa mkono na angalau wapigakura milioni moja, tunapanga kukusanya sahihi milioni nne kwa wiki moja,” Bw Waweru akasema.

Mbunge huyo wa zamani wa Dagoreti Kusini ambaye alikuwa ameandamana na Bw Mohammed na wanachama wengine wa sekritariati ya shughuli hiyo, alisema mswada wa marekebisho ya Katiba 2020 sasa uko tayari.

“Wiki jana, tuliahirisha mchakato huo dakika za mwisho baada ya kugundua kuwa utayarishaji wa mswada haukuwa umekamilishwa na kuchapishwa,” akaeleza.

Bw Waweru alisema kuwa shughuli hiyo ambayo itaongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga haitaahirishwa tena.

Kuahirishwa kwa mchakato huo Jumatano jioni saa chache baada ya Rais Kenyatta kukutana na Naibu wake William Ruto kuliibua uvumi kwamba, Dkt Ruto ndiye aliyemshawishi kuchukua hatua hiyo “ili kutoa nafasi ya kujumuishwa kwa mapendekezo ya wadau wengine, wakiwemo viongozi wa kidini.”

Uzinduzi wa Jumatano utafanyika katika uwanja wa Jumba la Mikutano ya Kimataifa (KICC), Nairobi, maarufu kama COMESA GROUNDS.