Kimataifa

Kundi sasa lapinga Disney kumiliki “Hakuna Matata”

December 21st, 2018 2 min read

Na MASHIRIKA

KUNDI la watu limeanzisha mchakato mtandaoni kulazimisha kampuni ya Disney kuachilia rajamu ya maneno ya Kiswahili “Hakuna Matata.”

Maneno hayo ni maarufu Afrika Mashariki na Kusini, hasa Kenya, ambako yalitumiwa na bendi ya Them Mushrooms (Uyoga) 1982 katika wimbo wao, Jambo Bwana, na kuyafanya maarufu.

Them Mushrooms ni Wakenya kutoka Pwani na ni maarufu kwa wimbo huo. Bendi hiyo inashirikisha Teddy Kalanda, Henry Ndenge Saha na Ben Mutwiwa na huiba nyimbo za Chakacha, Benga na reggae, zaidi ya kuwa hutumbuiza watu kwa nyimbo zao za zamani.

Kwa muda mrefu, maneno hayo yalitumiwa na Wakenya kuwakaribisha wageni, hasa watalii, kutoka mataifa ya ng’ambo nchini.

Wimbo huo uliandikwa tena na kuimbwa na Elton Johns (The Lion King) mwaka wa 1994 hatua iliyoufanya maarufu ulimwenguni.

Wimbo huo ulitumika katika filamu ya Disney, The Lion King, mwaka huo ambapo kampuni hiyo ilichapisha rajamu maneno hayo kulingana na afisi ya leseni na rajamu ya Amerika.

Ombi hilo lilianzishwa na mwanaharakati wa Zimbabwe Shelton Mpala, na tayari lilikuwa limetiwa saini na watu 117,000 kufikia Alhamisi jioni.

Kulingana na Mpala, alianzisha ombi hilo, “Kwa lengo la kuvutia watu katika unyakuzi wa utamaduni wa Kiafrika na umuhimu wa kulinda urithi wa Kiafrika, utambulisho na utamaduni ili kuulinda dhidi ya kutumiwa vibaya na watu kujinufaisha na watu wengine.”

“Hii ni sanaa iliyoporwa na inayanufaisha makavazi na mashirika mengine na sio waanzilishi wake au watu yalikotoka maneno hayo,” alisema Mpala.

Disney ilikataa kujibu maswali ya wanahabari. Lakini Liz Lenjo, wakili wa haki za uvumbuzi na burudani kutoka Kenya anahitilafiana na ombi hilo.

Lenjo alisema, “Disney haijaiba chochote na hasira kuhusiana na rajamu hiyo haifai. Watu wanafaa kulaumu mitandao ya kijamii kwa kusambaza habari hiyo sana,” alisema Lenjo.

“Matumizi ya ‘Hakuna Matata’ na Disney hayaondoi thamani ya lugha. Raia wa Afrika Mashariki, au yeyote anayezungumza Kiswahili ulimwenguni, hawajakatazwa kutumia maneno hayo.”

Aliongeza kuwa, “Mazungumzo ya mtandaoni yamekuwa yakifanya mambo kuwa makubwa kutokana na kutoelewa sheria kuhusiana na uvumbuzi na falsafa kuhusiana na sheria inayosimamia haki za uvumbuzi na masuala mengine ya kutoa ulinzi.”

Filamu mpya ya “The Lion King” inatarajiwa kuanza kupeperushwa 2019.