Habari za Kitaifa

Kung’ata na kupuliza: Serikali kuajiri tena walimu wa JSS waliofutwa kwa kugoma


WALIMU 742 wa Shule Msingi (JSS) ambao kandarasi zao zilisitishwa hivi majuzi kwa kushiriki  mgomo sasa wanaweza kupumua baada ya Tume ya Huduma ya  Walimu (JSC) kuahidi kuwaajiri upya.

Hata hivyo, walimu hao wanagenzi lazima wakate rufaa kwa Tume ili iwasikilize kwa mujibu wa Sheria ya TSC.

Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC, Nancy Macharia aliwataka walimu ambao mwanzoni mwa muhula huu walifutwa kazi kwa kushiriki mgomo kukata rufaa kwa Tume ili waruhusiwe kusikizwa kwa mujibu wa Sheria ya TSC.

“TSC imewaarifu walimu 742 ambao kandarasi zao zilikatizwa hivi majuzi kwa kugoma mwanzoni mwa muhula huu kwamba wanaweza kukata rufaa kwa Tume ili wapewe fursa ya kusikilizwa kwa mujibu wa Sheria ya TSC,” akasema Bi Macharia.

Mwezi uliopita, maelfu ya walimu wa JSS waliokuwa kwenye mgomo tangu Aprili 17, 2024, walifuta mgomo hadi Julai 5, 2024.

Walimu hao wanagenzi waliamua kusitisha mgomo wao ili kusubiri Bunge la Kitaifa kupitisha bajeti.

Walimu hao 46,000 pia walimsihi mwajiri wao, kuwaajiri kwa masharti ya Kudumu na Pensheni.

Walimu hao waliohitimu waliajiriwa mwaka wa 2019. Kupitia msemaji wao wa kitaifa Bw Omari Omari, walimu hao wa JSS waliitaka TSC kuwapa barua za kuwaajiri kwa masharti ya Kudumu na Pensheni mara tu baada ya bajeti kupitishwa.

“Baada ya mkutano na viongozi wa Kaunti wa JSS, tuliidhinisha kusimamisha mgomo wetu ili kuruhusu Bunge kupitisha bajeti siku ya Alhamisi. Kufikia tarehe hiyo, tunapaswa kuwa tumepata mawasiliano kuhusu hali ya kuthibitishwa kwa walimu hao 46,000,” akasema Bw Omari.

Hata hivyo, Bi Macharia aliwahakikishia walimu wa JSS kwamba mipango inaendelea kuhakikisha wanaohudumu katika shule za umma wanapewa kazi kwa kandarasi ya kudumu na ya pensheni.

“Tuna imani kuwa fedha za kutosha zitatolewa kwa shughuli hiyo, katika mwaka huu wa kifedha,” alisema mkuu huyo TSC ambaye alizungumza wakati wa Muungano wa Wakuu wa Shule za Sekondari Kenya unaoendelea mjini Mombasa.

Bi Macharia aliwahakikishia wakuu hao kwamba katika Mwaka huu wa Fedha wa 2024/2025, TSC itapandisha vyeo walimu zaidi baada ya serikali kutenga Sh1 bilioni kwa shughuli hiyo.

Kwa jumla TSC imepandisha vyeo walimu 36,504 katika Mwaka huu wa Fedha na hivyo kufanya jumla ya waliopandishwa vyeo katika miaka mitano iliyopita kufikia 71,212.

“Tutapandisha vyeo walimu wa zaidi. Kama Wakuu wa Shule, nawaomba mhimize walimu wanaohitimu katika shule zenu kutuma maombi ya nafasi hizo mara nafasi za kazi zitakapotangazwa,” akasema Bi Macharia.