Habari MsetoSiasa

Kuniambia nitoe kafara ni upuuzi, Gavana Njuki aiambia Njuri Ncheke

April 2nd, 2019 1 min read

Na ALEX NJERU

GAVANA wa Kaunti ya Tharaka-Nithi, Muthomi Njuki, amewasuta wazee wa baraza la wazee wa Meru (Njuri Ncheke), wanaomtaka atoe kafara ya ng’ombe ili “kuondoa laana” ya wanawake waliovua chupi na kuzitupa nje ya ofisi yake.

Mwezi uliopita, wanawake kutoka maeneo bunge ya Chuka/Igambang’ombe, Maara na Tharaka, waliandamana nje ya afisi ya Bw Njuki mjini Kathwana, na kuzitupa chupi zao kwenye lango kuu la ofisi yake kwa madai kwamba amewakosea heshima.

Akizungumza katika kanisa la Weru PCEA katika eneobunge la Chuka/Igambang’ombe, Bw Njuki alisema wazee hao na wanawake wanatumiwa na wapinzani wake wa kisiasa kumtisha na kumharibia sifa.

Alisema wale ambao walitupa chupi kwenye lango lake la ofisi yake walikuwa wametumwa na wapinzani wake, na kwamba ‘laana’ yao haimtishi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Njuri Ncheke katika Kaunti ya Tharaka-Nithi, Kangori M’Thaara amesisitiza kwamba ikiwa laana hiyo haitaondolewa kwa njia ya kafara, kuna uwezekano wa Bw Njuki na serikali yake kwa jumla kupatwa na mikosi mingi.

Gavana Njuki alisema rafiki zake wa karibu ambao walimsaidia katika kampeni ya 2017, ndio wanaowachochea wazee na wanawake hao baada yake kukataa kuwapatia pesa za umma.

“Wazee hao wanatumiwa na marafiki ambao wamegeuka maadui baada ya mimi kukataa na mali ya umma,” alisema Bw Njuki.

Alisema pia kuna uvumi kuwa anatoka maeneo ya Mbeere katika Kaunti ya Embu.

Akisisitiza umuhimu wa utakaso, Bw Kangori alisema kwa mujibu wa mila ya Ameru, wanawake wakivua nguo na kuonyesha sehemu zao za siri ilikuwa ni laana kali sana.