Kunihusisha na ufisadi kutafeli kwani Wakenya si wajinga-  Waiguru

Kunihusisha na ufisadi kutafeli kwani Wakenya si wajinga- Waiguru

Na CHARLES WASONGA

GAVANA wa Kirinyaga Anne Waiguru ametaja ripoti zinazosema kuwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imekamilisha uchunguzi kuhusu madai kuwa alipora fedha za umma katika serikali kama njama ya kuzuia wanasiasa kujiunga na chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Hata hivyo, Alhamisi alisema njama hiyo inayohusishwa na siasa za urithi wa urais zitafeli “kwa sababu Wakenya sio wajinga na kuna Mungu mbinguni”.

Bi Waiguru alisema hayo kufuatia ripoti iliyochapishwa katika gazeti moja la humu nchini Alhamisi kwamba EACC imekamilisha uchunguzi dhidi yake na kuwasilisha faili kwa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) ili afunguliwe mashtaka.

“Hakika, saa 48 baada ya sisi kuhamia UDA na sasa haya yanatokea. Kama kiongozi anayeheshimu utawala wa sheria nasikitishwa na hatua hii. Lengo lake ni kuwavunja moyo wale ambao wanapanga kuhamia UDA na kushawishi siasa za urithi. Njama hii itafeli. Wakenya sio wajinga. Kuna Mungu mbinguni,” Bi Waiguru akaandika katika ukurasa wake wa Facebook.

Kulingana na ripoti hiyo, Gavana Waiguru anatuhumiwa kuiba karibu Sh10 milioni kama marupurupu ya usafiri kwa madai kuwa alisafiri kwenda mataifa ya Amerika, Uingereza, Ufaransa, Morocco miongoni mwa mataifa mengine kwa ziara rasmi ya kikazi mnamo 2018.

Bi Waiguru pia ametuhumiwa kwa kupanga kulipa Sh52.8 milioni kinyume cha sheria kwa kampuni moja ya usoroveya kwa kugawanya ardhi ya mpango wa makazi ya New South Ngariama Scheme mnamo 2006.

Kampuni hiyo kwa jina, GeoAcres Survey Limited, inamilikiwa na aliyekuwa mbunge wa Kirinyaga ya Kati Joseph Gitari na mkewe Edith Gitari.

Inadaiwa kuwa wamiliki hao hawakuwa na mkataba na aidha Serikali ya Kaunti ya Kirinyaga au iliyokuwa Manisipaa ya Kirinyaga.

Kulingana na ripoti hiyo huenda Gavana Waiguru akashtakiwa pamoja na Afisa Mkuu wa Fedha katika serikali ya kaunti ya Kirinyaga Mugo Ndathi, Spika wa Bunge la Kaunti hiyo Anthony Gathumbi, kiongozi wa wengi katika bunge hilo James Murango na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge hilo David Mathenge.

Hawa wote waliandamana na Gavana Waiguru katika makazi rasmi ya Naibu Rais William Ruto Jumanne alipopokewa rasmi baada ya kugura Jubilee na kujiunga na UDA.

Duru zasema kuwa huenda wote hao wakakamatwa wiki ijayo.

Mnamo Septemba 9, mwaka huu Gavana Waiguru alifika katika makao makuu ya EACC ambapo alihojiwa kuhusiana na sakata hizo.

Hata hivyo, baada ya kudadisiwa kwa saa kadhaa, Gavana Waiguru alidai tume hiyo inaingiliwa kisiasa kumhangaisha na kuzima ndoto yake ya kuhifadhi kiti chake cha ugavana 2022.

“Ni wazi kuwa EACC inatumiwa kututisha ili tunyamaze licha ya kwamba wafuasi wetu wangali na imani katika utendakazi wetu,” akaeleza.

You can share this post!

Papa Francis ateua Askofu Anyolo kumrithi Njue

Raila na Ruto wachuuza asali chungu

T L