Habari Mseto

Kuolewa kulinisaidia kutoroka mauti msituni Shakahola

April 18th, 2024 2 min read

NEHEMIAH OKWEMBAH NA VALENTINE OBARA

KWA Bi Veronica Amanya, 21, uamuzi wa kuolewa baada ya kuhamia Msitu wa Shakahola na baadhi ya jamaa zake ndio ulimwokoa kutoka katika hatari ya kifo.

Veronica alikuwa amewasili na babake, mamake, mjomba na ndugu zake sita Malindi, Kaunti ya Kilifi, wakiwa waumini wa Kanisa la Good News International Ministries ambalo linahusishwa na mhubiri mwenye utata Paul Mackenzie, kabla ya kupelekwa katika Msitu wa Shakahola pamoja na waumini wengine.

Akiwa msituni, anasema wote walikuwa wakifanya ibada ya mfungo lakini hatimaye alitoroka akiwa anafanya kazi katika shamba lililopo katika ardhi ya Chakama iliyo ndani ya Msitu wa Shakahola na kwenda kuolewa na mwanamume aliyejuana naye.

“Tulikaa Malindi kwa siku tatu kabla ya kupelekwa Shakahola. Haikuwa rahisi kutoroka. Mara nyingi nilifikiria kurudi huko msituni lakini watu ambao nilikuwa nikiishi nao walinishawishi nisirudi,” akasema.

Veronica alizungumza katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi mnamo Jumanne, alipokuwa ameandamana na wanafamilia wengine kuchukua miili ya jamaa zao watatu waliokufa Shakahola kwa minajili ya mazishi.

Watatu hao ni miongoni mwa ndugu zake sita waliofariki katika mfungo huo uliosababisha vifo zaidi ya 430. Serikali hadi sasa imeweza kutambua karibu watu 34 pekee kupitia uchunguzi wa sampuli za DNA.

Veronica alisema kwamba, amewasamehe wazazi wake kwa kuisababishia familia mateso.

“Nina furaha sasa ndugu zangu wanaenda kuzikwa. Baba yangu alituleta Malindi ambapo tulichukuliwa na kupelekwa Shakahola.

Kilichoniokoa ni kwa sababu niliolewa huko Chakama karibu na Shakahola,” akasema.

Kulingana na shangazi yake, Bi Debora Amanya, anayetoka Luanda, Kaunti ya Vihiga, ndugu zake wawili walisafiri kutoka Nairobi hadi Malindi pamoja na watoto wao ili kujiunga na Bw Mackenzie ambaye alikuwa ametoka tu kufunga kanisa lake la Good News International (GNI) baada ya shinikizo kutoka kwa serikali na sehemu ya viongozi wa eneo la Malindi.

Wawili hao walikuwa wanachama wa tawi la GNI Jogoo Road tangu 2019 na kanisa lilipofungwa Desemba mwaka uo huo, walikaa kwa muda kabla ya kuuza mali zao zote eneo la Kasarani jijini Nairobi na kuelekea Malindi ambako Mackenzie alikuwa akiishi.

“Ndugu zangu wawili walifika Malindi na yule mkubwa alibeba mkewe na watoto saba na kati ya watoto hao, sita walikufa huko Shakahola na mmoja alinusurika baada ya kutoroka msituni,” alisema Bi Amanya.

Aliongeza kuwa, kakake mkubwa, Enos Amanya na mkewe, Ann Anyoso Alukhwe na mdogo wake, David Ambwaya Amanya, walikamatwa na wanakabiliwa na mashtaka mbalimbali pamoja na Mackenzie.

Mackenzie na washukiwa wengine 94 wamekanusha mashtaka yote dhidi yao, kuanzia ukiukaji wa haki za watoto hadi mauaji.

Alisema endapo jamaa zao walio kizuizini wataachiliwa huru, familia yao haingependa warudi nyumbani.

Mnamo Jumanne, familia tatu tofauti zilipokea miili saba ya waathiriwa wa vifo vya Shakahola.

Serikali iliwasaidia kusafirisha miilii hiyo hadi Kaunti za Uasin Gishu, Vihiga na Busia kwa mazishi.

Miili hiyo iliachiliwa na maafisa wa upelelezi wakiongozwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Kuchunguza Mauaji katika Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), Bw Martin Nyuguto, ambaye pia aliandamana na wanafamilia hao kwenye msafara wao.