Makala

Kuota jua kuna faida tele

June 25th, 2020 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

TUNALIONA jua kila siku likiangaza kutoka upande wa Mashariki na kutua upande wa Magharibi kila siku.

Kwa hakika kuna umuhimu mkubwa wa jua kwa mimea na viumbe vingine akiwemo binadamu.

Kuua bakteria

Miale ya jua inaweza kutumiwa kuua bakteria mbalimbali katika majeraha na ngozi. Tiba hii iligunduliwa na mshindi wa tuzo ya Nobel Niels Finsen.

Tiba hii ilitumiwa kuponya vidonda vya wanajeshi wa Kijerumani baada ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia.

Huondoa msongo wa mawazo

Inakadiriwa mtu anapokuwa penye miale ya jua, hupata kiasi kikubwa cha kemikali. Hivyo, kukosa jua kunasababisha tatizo linalofahamika kama vile Seasonal Affective Disorder (SAD). Hii SAD ni aina fulani ya msongo.

SAD hutokea mara nyingi kwa watu wengi kipindi cha masika au kwa wale wanaokaa ofisini muda mrefu. Hivyo, kuota jua kutakuongezea kemikali muhimu na kukuepusha na tatizo la Seasonal Affective Disorder (SAD).

Huzuia shinikizo la damu

Kemikali ya nitric oxide ambayo hukabili shinikizo la damu huingia kwenye damu pale mwili unapopigwa na miale ya jua.

Ni wazi kuwa jua haliboreshi afya pekee, bali huima maisha kwa kumwepushia mtu hatari ya kifo kinachoweza kutokana na shinikizo la damu.

Huboresha kinga ya mwili

Kukaa kwenye jua la wastani huwezesha uzalishaji wa seli nyeupe za damu ambazo huukinga mwili dhidi ya maradhi.

Hupunguza lehemu (cholestrol)

Jua linapopiga ngozi ya mwanadamu, hubadili lehemu iliyoko kwenye ngozi na kuifanya kuwa homoni ya steroid pamoja na baadhi ya homoni nyingine muhimu katika uzazi.

Hivyo kukaa palipo na miale ya jua hakupunguzi tu lehemu bali huzalisha pia homoni muhimu katika mwili wa binadamu.

Husaidia ukuaji wa watoto

Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa jua ni muhimu sana hasa kwa ukuaji wa watoto wadogo. Hivyo, kumweka mtoto nje ili apate angalau kiasi fulani cha mwanga wa jua kutaboresha afya na ukuaji wake.

Huongeza kiwango cha oksijeni mwilini

Jua linapoupiga mwili wako, linafanya seli nyekundu za damu kuweza kubeba na kusafirisha kiwango kikubwa zaidi cha oksijeni. Hili litapelekea kuwepo kwa kiwango kizuri cha oksjeni kwenye mwili wako.

Huimarisha mifupa

Inafahamika wazi kuwa jua ni chanzo cha upatikanaji wa vitamini D ambayo huuwezesha mwili kufyonza madini ya calcium na phosphorus yanayoimarisha mifupa.

Inaelezwa pia vitamini D3 inayozalishwa wakati wa uzalishaji wa vitamini D, husaidia kuzuia kuvunjika kirahisi kwa mifupa hasa kwa watu wenye umri mkubwa.