Kimataifa

Kupanga uzazi kunaipunguzia TZ watu, Magufuli aonya wanawake

September 12th, 2018 1 min read

BBC NA PETER MBURU

DAR, TANZANIA

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amewataka wanawake nchi hiyo kukoma kutumia dawa za kupanga uzazi na kuzaa watoto wengi, akisema nchi hiyo ina uhitaji wa watu zaidi.

Lakini semi hizo fupi za Rais wa misimamo mikali zilivutia ukosoaji kutoka kwa baadhi ya viongozi wa taifa hilo lenye zaidi ya watu 50milioni.

“Wanawake sasa wanaweza kuwacha kutumia mbinu za kupanga uzazi,” alisema Bw Magufuli, Rais wa muhula wa kwanza.

Bw Magufuli alisema hivyo alipokuwa eneo la Meatu Jumapili, akisema watu wanaotumia njia za kupanga uzazi ni wavivu, akinukuliwa na gazeti moja la nchi hiyo kuwa “hawataki kutia bidii kulisha familia kubwa.”

“Nimezuru mataifa mengi Uropa na nimeona mathara ya mbinu za kupanga uzazi, mataifa mengine sasa yana upungufu wa watu,” akasema.

Mbunge wa upinzani Cecil Mwambe alikashifu semi za Rais huyo, akisema zilikinzana na sheria ya afya ya nchi hiyo kwani takriban asilimia 49 ya raia wake ni masikini.

Tanzania inaorodheshwa kati ya mataifa ambayo wanawake huzaa sana, kwa kawaida kila mwanamke akiwa na watoto watano.

Siku moja baada ya semi za rais, spika wa bunge la nchi hiyo Job Ndugai naye alipiga marufuku wabunge wanawake kujipodoa kwa kucha na nyusi za kupachika wakiwa bungeni, akisema ni kwa sababu za kiafya.

Mnamo 2016, Rais huyo anaripotiwa kuwahi sema maneno ya aina hiyo alipoanzisha mradi wa shule za msingi bila malipo na kusema “Wanawake sasa wanaweza kutupilia mbali upangaji uzazi. Elimu ni ya bure sasa.”

Mwaka uliopita, Bw Magufuli alisema wasichana wanojifungua wakiwa shuleni wasiruhusiwe kurejelea elimu baada ya kujifungua.