Habari Mseto

Kupigia mbuzi gitaa: Madaktari wapuuza wito wa kurejea kazini kukabili wimbi la nimonia

April 10th, 2024 2 min read

NA WINNIE ATIENO

MADAKTARI katika Kaunti ya Mombasa wamepuuzilia mbali ombi la serikali ya Gavana Abdulswamad Nassir kurudi kazini ili kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa nimonia miongoni mwa watoto.

Jumatatu, serikali ya Kaunti ya Mombasa iliwaamrisha madaktari na maafisa wa kliniki walio likizoni na wale wanaoendeleza mgomo wao wa kitaifa kurudi kazini mara moja, ili kukabiliana na mlipuko wa nimonia miongoni mwa watoto.

Hata hivyo, wakuu wa chama cha madaktari nchini tawi la Pwani walikataa wito huo, wakisema mgomo huo uliitishwa na afisi yao ya kitaifa.

Kulingana na madaktari wa watoto katika Kaunti ya Mombasa, hospitali za kibinafsi zimekuwa zikitibu watoto wanaougua nimonia huku wengi wao wakilazimika kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kufuatia kudhohofika kwa hali yao ya afya.

Hata hivyo, ongezeko la idadi ya wagonjwa hao inazidi kuwatia wasiwasi wakuu wa afya katika kaunti hiyo.

Hali hii inazidi kuzorota kufuatia mgomo wa kitaifa wa madaktari nchini.

Kwenye mkutano na chama cha madaktari nchini, wakuu wa serikali ya Gavana Nassir, waziri wa afya wa kaunti, Dkt Swabah Omar, alikisihi chama cha madaktari kusitisha mgomo huo.

“Tulimwambia mgomo utaendelea kwa sababu uliitishwa na makao yetu makuu. Twajua kuna hali tete Mombasa kufuatia mlipuko huo ambao unadaiwa kusababisha maafa, lakini mgomo utaendelea,” alisema afisa mkuu wa chama hicho tawi la Pwani, Dkt Gharib Salim Ali.

Mnamo Aprili 8, 2024, Dkt Omar aliandika barua ya dharura katika idara yake ya afya akiwasihi maafisa wa kliniki na madaktari kurudi kazini mara moja kufuatia mlipuko huo.

“Kuna ongezeko la huduma za kiafya katika hospitali zetu kufuatia janga la nimonia na maradhi mengine. Ninawaagiza madaktari na maafisa wa kliniki walioko likizoni kurudi kazini mara moja kukabiliana na mlipuko huu,” aliagiza Dkt Omar.

Daktari wa watoto wa Hospitali ya Aga Khan mjini Mombasa, Dkt Hemed Twahir, alisema katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, wamekuwa wakiuguza maradhi ya nimonia na kuendesha miongoni mwa watoto.

“Tumenakili ongezeko la kuendesha na dalili za nimonia ikiwemo kushindwa kupumua miongoni mwa watoto. Tumelazimika kuwalaza katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa sababu ya kudhoofika kwa afya,” alisema Dkt Twahir.

Akiongea na Taifa Leo, Dkt Twahir alisema wagonjwa wengine wamelazimika kuwekewa mashini ya kusaidia kupumua.

Daktari huyo aliwasihi wazazi kuhakikisha watoto wanaoshwa mikono kwa sabuni mara kwa mara, wanakunywa maji safi yaliyochemshwa au kutiwa dawa.

Alionya kuwa hali itazidi kudhoofika kufuatia mvua inayoendelea kunyesha hasa ugonjwa wa kuendesha.

“Mtoto akiwa na joto mwilini, akikohoa, na kuendesha au kuwa na changamoto kupumua tafadhali nenda hospitalini. Msinunue dawa kwenye duka za dawa,” aliongeza.

Vilevile, Dkt Twahir aliwasihi wazazi kuhakikisha watoto wachanga wanapewa chanjo ya nimonia wakiwa umri wa wiki sita, wiki 10 na wiki 14 ili kuzuia ugonjwa huo.