Habari

Kuppet yaelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya elimu Kaskazini Mashariki

February 22nd, 2020 1 min read

Na BRENDA AWUOR

BAADHI ya viongozi wa walimu sasa wanaiomba Tume ya Kuajiri Walimu Nchini (TSC) na serikali nzima kuwahakikishia usalama walimu katika maeneo ya Kaskazini Mashariki.

Katibu mkuu wa Kuppet, Bw Akelo Misori, anawakashifu viongozi kutoka maeneo ya Kaskazini Mashariki kwa kile anasema ni wao kutojali masilahi ya walimu licha ya hali mbaya ya usalama.

Hata amethubutu kusema TSC inafaa kuwapa walimu kutoka Kaskazini Mashariki bunduki kujikinga.

Akihutubu katika mkutano uliowaleta pamoja viongozi wa walimu na walimu wanawake ili kukuza ujuzi wa uongozi, Misori ameliangazia swala la usalama kama changamoto kuu inayokumba walimu hasa katika maeneo ya Kaskazini Mashariki.

Amependekeza walimu maeneo hayo wapewe bundiki jambo ambalo litafanya magaidi kuhofia kuwafikia.

‘’TSC inapaswa kuwapa walimu hao bundiki kama njia ya kujikinga dhidi ya magaidi na wapiganaji,’’ amesema Misori.

Mwenyekiti wa Kuppet Bw Omboko Milemba, aidha amependekeza sheria ya TSC ya kutoza kila mwalimu Sh6,000 wanapopewa mafunzo ya kuongeza maarifa kuhusu mfumo mpya wa elimu unaozingatia uamilifu (CBC) ifutwe kwa kuwa inawaumiza walimu.

“Walimu hawastahili kutozwa pesa yoyote wanapopewa maarifa mapya; ni jukumu la tume kugharimia mahitaji yote kwani kufaidika kwa wasomi ni kufaidika kwa serikali bali si walimu,’’ ameeleza.