Habari Mseto

Kuppet yalaumu wanasiasa kuhusu walimu kuvamiwa

February 17th, 2020 2 min read

Na OUMA WANZALA

CHAMA cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo Anuwai (KUPPET) kimetoa wito kwa wanasiasa kutoka Kaskazini Mashariki wakome kuchochea uvamizi dhidi ya walimu ambao si wa asili ya eneo hilo.

Walimu wamekuwa wakitoroka eneo hilo kutokana na ukosefu wa usalama unaosababishwa na uvamizi wa mara kwa mara wa makundi ya kigaidi.

Katibu Mkuu wa Kuppet Akelo Misori, Jumatatu alitoa wito kwa viongozi washirikiane na serikali kutatua masuala ya ukosefu wa usalama na kuwazima magaidi badala ya kuwalaumu walimu wanaotorokea usalama wao.

“Kama chama tunasikitikia uvamizi wa mara kwa mara dhidi ya walimu ambao si wenyeji wa Kaskazini Mashariki. Wanasiasa wanafaa wapendekeza suluhisho badala ya kuwakashifu,” akasema Bw Misori.

Afisa huyo alisema kwamba chama hicho hakitafurahi kushiriki maombolezi ya hata mwalimu mmoja ambaye atafariki kutokana na uvamizi wa makundi ya kigaidi.

Isitoshe, Bw Misori aliongeza kwamba chama hicho kinaunga mkono uamuzi wa Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) kuhakikisha hali ya usalama kwa walimu inapewa kipaumbele.

Mwezi uliopita, TSC iliwahamisha zaidi ya walimu 1,000 ambao si wenyeji wa kaunti za Wajir, Mandera na Garissa kufutia uvamizi wa kigaidi uliowalenga.

Hatua ya TSC ilichochewa na kisa cha Januari 13 ambapo wahalifu waliojihami vikali waliwaua walimu watatu wa kiume katika kituo cha Kamuthe.

Hata hivyo, viongozi wa eneo hilo walipinga hatua ya TSC wakisema imelemaza shughuli za masomo katika shule za umma za eneo hilo.

Viongozi hao walioongozwa na Kiongozi wa wengi kwenye Bunge la Kitaifa Aden Duale wanataka tume na Waziri wa Elimu Profesa George Magoha wafike mbele ya bunge ili waeleze mikakati waliyoweka kuhakikisha shughuli za masomo zinarejelewa kama kawaida.

Bw Duale aliahidi kutafutu suluhu kwa tatizo la walimu wasioasili kuvamiwa na wapiganaji wa Al Shabaab huku magavana Ali Korane (Garissa), Ali Roba (Mandera) wakisema eneo hilo kwa sasa linakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu.

“Tuna watoto walioko shuleni lakini hakuna walimu wa kuwapa mafunzo. Hii ni kuwanyima watoto wetu haki ya kikatiba ya kupata elimu,” akasema Bw Korane.

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa TSC Beatrice Wababu alithibitisha kwamba walimu waliohamishwa wamepelekwa maeneo salama.