Habari Mseto

KUPPET yamtetea mwalimu aliyedaiwa kutunga mimba mwanafunzi

June 24th, 2019 2 min read

NA PHYLLIS MUSASIA

CHAMA cha Walimu wa Shule za Upili (KUPPET) tawi la Nakuru  sasa kinataka mwalimu aliyewachishwa kazi katika eneo la Kuresoi Kaskazini, kwa madai kuwa alimtia mimba mwanafunzi wa kidato cha nne mwaka uliopita, arejeshwe kazini mara moja.

Kulingana nao, mwalimu Philip Langa’t hana hatia na kufurushwa kwake kulizingatia madai ya uongo yaliokosa kuthibitishwa.

Kupitia kwa katibu mtendaji wa chama hicho Bw Eliud Wanjohi, Tume ya Kuwaajiri Walimu nchini (TSC) inapaswa kuamuru kurejeshwa kazini kwa Bw Langa’t na pia kufidiwa kwa muda wote ambao amekuwa nje.

“Muungano huu umekuwa ukifuatilia kwa karibu sana kesi ya Bw Langa’t tangu madai ya kumnajisi mwanafunzi wa shule yalipoibuka mwaka uliopita. Na kulingana na ripoti ya ofisi ya upelelezi wa maswala ya jinai ya Olenguruone; Kuresoi, ni wazi kuwa mwalimu huyu hana hatia haswa baada ya ripoti ya vinasaba vya chembechembe za DNA kuonyesha kuwa yeye si baba wa mtoto aliyezaliwa,” ikasoma baadhi ya taarifa hiyo.

Aidha, uchunguzi huo wa DNA uliofanywa zaidi ya mara tatu katika mahabara ya serikali kule Kisumu, ulimpa mwalimu Langa’t afueni tosha na kumuondolea hatia.

Kulingana na ripoti ya upelelezi wa kesi hiyo kwenye stakabadhi nambari 2/2019 katika ofisi ya Kuresoi, Bw Langa’t alitengwa na madai hayo huku mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Mawingu kwenye eneo Bunge la Kuresoi Kaskazini Bw Wilson Salpei akipatikana na hatia ya kushirikiana na watu wegine watatu kutoa habari za uongo kwa maafisa wa polisi na pia tume ya TSC.

Hata hivyo, muungano wa KUPPET ulisema kwamba ni kufuatia ripoti hiyo ya upelelezi ndipo ilibainika wazi kuwa shutuma dhidi ya Bw Lang’at ziliibuka kufuatia malumbano ya uhasama kati yake na mwalimu mkuu Bw Salpei.

Muungao huo unaitaka pia tume ya TSC kumchukulia hatua kali za kinidhamu Bw Salpei kwa kutumia mamlaka yake vibaya kukandamiza mdogo wake.

“Licha kuwa Bw Salpei anakabiliwa na makosa ya jinai ya kutoa habari za uongo kwa polisi na pia tume ya TSC dhidi ya Bw Langa’t, tume ya TSC inapaswa kumchukulia hatua kali za kinidhamu kwa kumwaribia hadhi mdogo wake na pia kumsababishia hasara kubwa ya kifedha baada ya kupoteza kazi yake,” ikaeleza taarifa hiyo ya KUPPET.