Habari Mseto

Kura: Seneta ataka majina bandia yawe halali debeni

November 1st, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

KARATASI za kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2022 zitajaa majina bandia ya wanasiasa ikiwa mswada wa kutaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itambue majina hayo kuwa halali utapitishwa kuwa sheria.

Katika miaka iliyopita, wanasiasa wengi walilazimika kufuata hatua zote za Sheria ya Usajili wa Watu zinazohitajika kwa raia yeyote kuhalalisha majina yao ya kubandikwa.

Seneta wa Nyeri, Bw Ephraim Maina ambaye amependekeza mswada huo alisema sheria za kubadilisha majina huhitaji mtu kutumia muda mrefu mno, hivyo kulazimu wanasiasa wengine kutumia majina yasiyofahamika kwa wafuasi wao kwenye karatasi za uchaguzi.

“Lengo kuu la uchaguzi ni kuhakikisha kwamba wapigakura wanachagua viongozi wanaowataka katika mazingara huru na ya haki. Kwa msingi huu, uwezo wa kutambua jina la mgombeaji ni hitaji muhimu kutimiza uchaguzi huru na wa haki na unafaa kufanikishwa kikamilifu,” akasema.

Mfano wa viongozi wanaokumbwa na changamoto kuhusu majina yao ni mgombeaji ubunge kwenye uchaguzi mdogo Kibra kwa tikiti ya Chama cha ODM, Bw Benard Otieno Okoth ambaye anafahamika zaidi kama Imran.

Wanasiasa wengine ambao wafuasi wao wamewabandika majina yaliyopata umaarufu kitaifa lakini hawayatumii kihalali ni Rais Uhuru Kenyatta (Kamwana), Kiongozi wa ODM Raila Odinga (Baba), Naibu Rais William Ruto (Hustler), Gavana wa Mombasa Hassan Joho (Sultan) na mwenzake wa Kirinyaga Anne Waiguru (Minji Minji).

Wengine ni Kiongozi wa Chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi (Madividii), Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula (Weta) na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Nairobi Esther Passaris (Mama Taa).

Baadhi ya wanasiasa walioamua kuhalalisha majina yao bandia kupitia kwa sheria za sasa ni Gavana wa Nairobi Gideon Mbuvi Kioko (Mike Sonko), mwenzake wa Kiambu Ferdinand Ndung’u Waititu (Baba Yao), Gavana wa Murang’a Francis Mwangi (Mwangi wa Iria) na aliyekuwa Mbunge wa Mukurweini Godfrey Kariuki Mwangi (Kabando wa Kabando).

Pia kuna Seneta wa Kiambu Paul Njoroge Kimani (Kimani Wamatangi), Mbunge wa Thika Mjini Patrick Kimani Wainaina (Jungle), mwenzake wa Kabete James Githua Kamau (Wamacukuru) na wa Embakasi Kusini Paul Ongili Owino (Babu Owino).

Katika pendekezo lake, Seneta Maina anasema si haki kuzuia wagombeaji viti tofauti vya kisiasa kutumia majina ambayo wafuasi wao wanafahamu zaidi bila sababu za msingi.

Vile vile, anasema hali hii hunyima wapigakura haki yao ya kikatiba kujichagulia viongozi kwa njia huru na ya haki kwani wanaweza kuchanganyikiwa.

Hata hivyo Bw Maina alisema uamuzi wa mwisho kuhusu kama mgombeaji ataruhusiwa kutumia jina lake la kubandikwa utakuwa mikononi mwa IEBC.

“Ili kuhakikisha kwamba uhuru huu (wa kutumia jina bandia) hautatatiza mipango ya kuwezesha uchaguzi kufanywa kwa njia huru na ya haki, IEBC itakuwa na mamlaka kuamua kama itaidhinisha mwanasiasa kutumia majina hayo uchaguzini,” akasema.

Kulingana naye, hili ni jambo linaloathiri viongozi wote wa kisiasa wakijumuisha madiwani, maseneta, wabunge na magavana.