Habari MsetoSiasa

Kura ya maamuzi haiwezi kufanyika – Murkomen

October 11th, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen amesema marekebisho ya katiba kupitia kura ya maamuzi hayatafanyika katika kipindi cha miaka minne ijayo  kwani kuna masuala mengi ambayo serikali inapasa kushughulikia.

Akiongea Jumanne usiku kwenye mahojiano katika runinga ya NTV seneta huyo wa Elgeyo Marakwet alisema kuna mapendekezo mengi kwa hivyo makubaliano kuhusu swali la kupigiwa kura yatachukua muda mrefu.

Murkomen kufanyika kwa kura ya maamuzi kutayumbisha ajenda ya maendeleo ya serikali haswa Agenda Nne Kuu ambazo serikali imeanza kutekeleza.

“Kubadilishwa kwa Katiba hakutaleta ujira au maendeleo hau uwakilishi sawa watu wa makabila yote serikalini. Miito hii ya marekebisho ya katiba inatokana na changamoto za kiuchumi zinazowaathiri Wakenya sasa. Wanahadaiwa kuamini kuwa chimbuko la hali hiyo ni idadi kubwa ya wabunge au madiwani uwepo wa bunge la seneti,” akasema Murkomen.

Alikubali kuwa kuna masaula fulani kwenye Katiba ambayo yanapaswa kufanyiwa mabadiliko japo kwa njia ya mwafaka. “Hatutaki wanasiasa fulani kuanza kupandisha joto la kisiasa nchini mwaka mmoja baada ya Wakenya kupiga kura na kuwachagua viongozi wao,”

“Lakini ikiwa Wakenya watakubaliana kubadilisha katiba, binafsi sitapinga ila nitawashauri wanasiasa kukoma kutumia suala hilo kujitafutia umaarufu kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Viongozi wa upinzani Raila Odinga na Kalonzo Musyoka wamekuwa wakiunga mkono mageuzi ya Katiba wakipigia debe kuanzishwa kwa mfumo wa ubunge.

Baraza la Kitaifa la Makanisa ya Kiprotestanti (NCCK) pia linapendekeza kubuniwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu na manaibu wake wawili.