Habari MsetoSiasa

Kuria ajiona kama 'zawadi' kwa Wakenya

July 21st, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MBUNGE wa Gatundu Kusini sasa anadai kuwa ndiye zawadi ya Kenya kutoka kwa Mungu, ambayo itawashikanisha Wakenya wote.

Akizungumza alipokuwa eneo la Magharibi Jumapili, Bw Kuria alisema kuwa anaandaa mkutano mkubwa katika eneobunge lake, ambapo atawaalika viongozi wote wakuu kisiasa, kwa lengo la kuwapatanisha.

Mbunge huyo alisema umoja wa kitaifa unhitajika kwa sasa, akionyesha kuwa yuko tayari kuongoza juhudi hizo.

“Nitaitisha mkutano mkubwa sana huko Gatundu na ninawaomba Baba 9Raila Odinga, Musalia Mudavadi, William Ruto, Uhuru Kenyatta wote waje huko,” Bw Kuria akasema.

“Nitakuwa mstari wa mbele kushikanisha Wakenya wote. Mimi ndio ile zawadi Mungu aliwapa kuwashikanisha,” mbunge huyo akaendelea kusema, akisifia mkutano anaopanga kuuandaa.

Mbunge huyo mtatanishi aliendelea kusema kuwa kuandaa mkutano huo kutakuwa kuendeleza ajenda ya Rais wa kwanza wa taifa Mzee Jomo Kenyatta, ambaye alitaka Wakenya wote wawe pamoja.

“Mimi ndiye nimekalia kiti ambacho kilikuwa kimekaliwa na Jomo Kenyatta, hata hivi viatu mnaona sio vya kununua, ni Jomo aliniachia,” akasema, akiongeza jinsi Mzee Kenyatta alikuwa na mapenzi ya kutaka Kenya ikiwa pamoja.