HabariSiasa

Kuria ajuta kumsimanga Raila

July 23rd, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA

MBUNGE wa Gatundu Kusini, Moses Kuria, amefichua kuwa licha ya tabia yake ya kumkashifu kiongozi wa upinzani Raila Odinga, waziri huyo mkuu wa zamani alimuokoa wakati mmoja na hata kumlipia wakili wa kumtetea kortini.

Kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2017, Bw Kuria alikuwa mmoja wa wanasiasa wa chama cha Jubilee aliyemkosoa vikali Bw Raila.

Aliwahi kuchunguzwa kwa madai ya kuchochea chuki kufuatia matamshi ya kumdunisha Raila na familia yake.

Hata hivyo, baada ya muafaka wa Raila na Rais Uhuru Kenyatta, Bw Kuria alikuwa mmoja wa wanasiasa wa kwanza wa Jubilee kumtembelea Bw Raila.

Mnamo Jumamosi, Bw Kuria alifichua kwamba Raila alimsaidia sana alipofukuzwa chuo kikuu chini ya utawala wa Rais Mstaafu Daniel Moi na kutaja tofauti zao za kisiasa kabla ya Raila na Rais Uhuru Kenyatta kusalimiana kama upumbavu.

“Kwa sababu ya muafaka, leo nimekaribishwa kwa moyo mkunjufu na watu wa Kisumu. Nimeshangaa kwa sababu ya tofauti za kipumbavu za kisiasa ambazo zimekuwa zikitugawanya,” Kuria alisema.

“Nilikuwa kiongozi mkakamavu wa wanafunzi katika chuo kikuu cha Nairobi na kwenye uchaguzi, tulishinda viti vyote na nikafukuzwa,” Bw Kuria alisimulia akiwa Nyakach kwenye hafla ya kumkaribisha nyumbani katibu wa wizara ya Teknolojia na Mawasiliano, Jerome Ochieng.

“Ni yeye ( Raila) aliyemtuma aliyekuwa seneta Otieno Kajwang ambaye aliniwakilisha mbele ya Jaji Gideon Mwera,” alisema. Marehemu Kajwang alikuwa wakili na mwandani wa Bw Raila.

Bw Kuria alisema kwamba jaji huyo alitoa agizo arejeshwe chuoni. Mbunge huyo alisimulia kwamba uhusiano wake na familia ya Jaramogi Oginga Odinga, baba ya Raila, ulianza kitambo.

Alikumbuka kwamba alipohudhuria mazishi ya Jaramogi 1994 nyumbani kwake Bondo na kwenye maadhimisho ya mwaka mmoja wa kifo chake 1995, walirushiwa gesi ya kutoa machozi kwa kucheza muziki.

Bw Kuria alisema wakati huo kulikuwa na muungano wa iliyokuwa mikoa ya Kati na Nyanza.

Alisema kama haungekuwa muafaka wa Raila na Rais Kenyatta hangekanyaga Nyanza kutokana uhasama uliotokana na uchaguzi mkuu uliopita.

“Punde tu baada ya salamu (za Raila na Uhuru), nilikuwa mtu wa pili kumtembelea Raila ili anieleze salamu hizo zilimaanisha nini. Aliniambia hazikuhusu siasa za urithi za 2022 au nyadhifa, bali lengo ni kuunganisha Wakenya,” alisema.

Alisema kutoka siku hiyo aliapa kuunga maridhiano na kuwataka Wakenya wote kukumbatia juhudi hizo.

Bw Kuria alisema ni wanasiasa wanaofaa kulaumiwa kwa shida zinazokumba Kenya.

Alisisitiza kwamba muafaka wa Raila na Uhuru utasaidia Kenya kuafikia Ajenda Nne Kuu za Maendeleo za serikali ya Jubilee.