Habari

Kuria apendekeza Murkomen ajiuzulu

September 20th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Gatundu Kaskazini Moses Kuria amemtaka Seneta wa Elgeyo-Marakwet Kipchumba Murkomen kujiuzulu wadhifa wake wa kiongozi wa wengi katika Seneti kutokana na matamshi yake kuhusu kuzimwa kwa mradi wa ujenzi wa bwawa la Kimwarer.

Akiongea na wanahabari katika majengo ya bunge Alhamisi Bw Kuria alisema Murkomen hafai kuwa kiongozi wa Jubilee katika seneti kwa sababu amefeli kudumisha heshima ya ofisi hiyo.

“Inasikitisha kuwa Bw Murkomen ameamua kuingiza ukabila kwa kila kitu, ikiwemo ripoti iliyoandaliwa na wataalamu,” akasema Kuria.

Mnamo Jumatano, Rais Uhuru Kenyatta alifutilia mbali mradi wa ujenzi wa bwawa la Kimwarer baada ya uchunguzi kubaini kuwa mradi huo haukuwa na manufaa yoyote.

Dakika chache baada ya Rais kutoa tangazo hilo Bw Murkomen alitoa taarifa akisema Rais Kenyatta aliongozwa na nia mbaya katika kutoa tangazo hilo.

“Kama ambavyo nimekuwa nikisema kila mara, kumekuwa na mpango wa kuua miradi mikubwa katika Kaunti ya Elgeyo-Marakwet. Uanachama wa kamati hiyo ya kiufundi hauakisi usawa kikabila na kimaeneo. Ni aibu kwamba Maringa, Matu, Mwangi na Muiruru ambao hawana uelewa au uhusiano na eneo hilo, walimpotosha Rais. Kamati hiyo ya kiufundi haikushauriana na yeyote kutoka Elgeyo-Marakwet,” akasema Bw Murkomen.

Haki

Alisema wanafanya mashauriano kama watu wa Elgeyo-Marakwet na watafanya kila wawezalo kuhakikisha wakazi “wanatendewa haki.”

Bw Kuria alisema ataitisha kuandaliwe mkutano maalum wa kundi la wabunge wa chama cha Jubilee ili kujadili mpango wa kumwondoa Murkomen kutoka wadhifa wa kiongozi wa wengi katika seneti.

Alisema matamshi ya seneta Murkomen yanaweza kusababisha uhasama wa kikabila baina ya Wakikuu na Wakalenjin