Habari MsetoSiasa

Kuria ashangaa kwa nini Matiang'i hajakamatwa kwa kusema Wachina watimuliwe

June 26th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MBUNGE wa Gatundu Kusini Moses Kuria Jumatano amekashifu hatua ya polisi kumkamata mbunge wa Starehe Charles Njagua ‘Jaguar’ kuhusiana na matamshi yake dhidi ya raia wa kigeni.

Akizungumza nje ya kituo cha polisi cha Nairobi Area ambapo Jaguar alifikishwa kuhojiwa baada ya kukamatwa, Bw Kuria alisema matamshi ya Jaguar hayakuwa na hatia yoyote, kwani ndio wito wa viongozi, kuwa raia wa kigeni ambao wanafanya kazi zinazoweza kufanywa na Wakenya warejeshwe makwao.

Bw Kuria alishangaa ni kwa nini Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiangi hajakamatwa, ilhali amekuwa akitoa matamshi sawa na hayo, kuwa raia wa kigeni wanaofanya kazi zinazofaa kufanywa na Wakenya watimuliwe.

“Hakuna tofauti na kile Matiang’i amekuwa akisema, kwa nini yeye hajakamatwa? Amekuwa akisema kuwa suala la raia wa kigeni kuja kufanya kazi zinazoweza kufanywa na Wakenya halikubaliki katika taifa lolote,” Bw Kuria akasema.

Alisema Dkt Matiangi amekuwa akisisitiza kuwa Wachina na raia wengine wa kigeni wanaofanya kazi za Wakenya wanafaa kutimuliwa, ilhali yeye hajawahi kukamatwa.

Mbunge huyo aliendelea kusema kuwa Wakenya pia wamekuwa wakihangaishwa nchini Tanzania, akirejelea kisa ambapo kuku wa wafanyabiashara kutoka Kenya waliripotiwa kuchomwa nchini humo.

“Kuna yeyote aliadhibiwa kwa kuchoma kuku wetu Tanzania? Magufuli aliathibu yeyote ama kumvamia kwa gesi za kutoa machozi?” akauliza Bw Kuria.

Wakiwa pamoja na mbunge wa Lang’ata Nixon Korir na wafuasi wa Bw Jaguar ambao walikuwa wamepiga kambi nje ya kituo hicho cha polisi, walivamiwa kwa gesi za kutoa machozi na polisi, wakati wafuasi hao walihimiza mbunge wao aachiliwe.