HabariSiasa

Kuria ataka bunge libuni wadhifa wa Waziri Mkuu

June 23rd, 2019 2 min read

Na ERIC WAINAINA

MBUNGE wa Gatundu Kusini Moses Kuria, ameunga mkono pendekezo la kubuniwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu na manaibu wawili lakisema hiyo ni kazi ya bunge.

Bw Kuria alisema kubuniwa kwa wadhifa huo ni njia moja ya kuhakikisha kuna uwakilishi serikalini na kukomesha uhasama wa kisiasa baada ya uchaguzi.

Mbunge huyo mbishi wa Jubilee aliunga mkono wito wa kubadilisha katiba lakini akasema baadhi ya mabadiliko yanapaswa kufanywa na bunge na yatakayobaki kwenye kura ya maamuzi itakayofanywa wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Kuria alisema waziri mkuu na manaibu wake wawili wanapaswa kutoka chama kimoja na kugombea uchaguzi mkuu kwa maana kuwa wagombeaji wa urais, wagombea wenza na wanaopendekeza kuwa waziri mkuu na manaibu wake wanapaswa kushiriki kampeni pamoja.

Hata hivyo, Bw Kuria aliyekuwa akiwasilisha maoni yake kwenye Kamati ya Maridhiano BBI iliyoandaa kikao katika chuo cha mafunzo anuwai cha Kiambu alisema mageuzi hayo hayahitaji kura ya maamuzi.

Kulingana na Bw Kuria, marekebisho hayo yanaweza kufanywa kupitia bunge na akawataka wanachama wa kamati kuhakikisha imepata imani ya Wakenya ili mapendekezo yao ya mwisho yaungwe na Wakenya wengi.

Aidha, mbunge huyo anapendekeza kuwe na upinzani utakaokuwa na baraza mwigo la mawaziri watakaolipwa na pesa za mlipa ushuru ili wachunguze serikali.

Alisema upinzani unapaswa kuwa na makali na unapaswa kuongozwa na wagombeaji wa urais wanaoibuka wa pili katika uchaguzi tofauti na sasa ambapo wanaoshindwa kwenye uchaguzi hupigwa na baridi ya kisiasa hadi uchaguzi mkuu unaofuatia.

“Kwa wakati huu hatuna upinzani na ni kweli ni wabunge wa upinzani wanaounga serikali. Tunapaswa kuwa na upinzani mwaminifu ambao utashirikisha wagombeaji wanaoshindwa kwenye uchaguzi wa urais ambao wataunda baraza la mawaziri kuchunguza serikali,” alisema Bw Kuria. Alipendekeza kuwa mawaziri wanafaa kuwa wabunge ili waweze kuwakilisha maslahi ya umma.

Mbunge wa Kiambu Mjini Jude Njomo alisema mbali na kamati huyo kuhakikisha kuna serikali inayowakilisha watu wote, inayowajibika kwa umma na kuhakikisha wameimarisha kiuchumi.