Habari Mseto

Kuria: Mimi ni wa pili kwa umaarufu Kisumu baada ya Raila

June 19th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MBUNGE wa Gatundu Kusini, Moses Kuria ameibua ucheshi baada ya kujigamba kuhusu umaarufu wake eneo la Luo Nyanza, hasa Kaunti ya Kisumu, akisema kuwa sasa ndiye wa pili kwa umaarufu baada ya kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga.

Alipokuwa akizungumza katika kipindi cha mahojiano katika runinga ya Citizen Jumanne usiku, Bw Kuria alielezea jinsi amekuwa akizuru Kisumu mara kwa mara, na kuwa hali hiyo imemjengea umaarufu.

Alisema hayo alipokuwa akieleza dhana yake kuhusu jinsi mirengo tofauti ya kisiasa imekuwa ikitafsiri muafaka baina ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga, ambao walianzisha Machi 9, 2018.

“Huwa ninazuru Kisumu mara kwa mara na nina umaarufu sana huko. Mimi ndiye wa pili kwa umaarufu Kisumu baada ya Raila Odinga,” Bw Kuria akasema, alipokuwa akieleza jinsi wafuasi wa Bw Odinga wanatafsiri muafaka.

Mbunge huyo wa chama cha Jubilee aliendelea kusema: “Kulingana na watu wa Nyanza, handisheki inamaanisha kuwa Raila atakuwa Rais, Uhuru awe Waziri Mkuu, kisha kina Kalonzo na Gideon Moi wapewe viti.”

Ajizolea umaarufu

Alisema kuwa amekuwa karibu zaidi na Bw Odinga na wafuasi wake ndipo akajua hayo, lakini akiongeza kuwa vilevile amejizolea umaarufu mkubwa Kisumu kutokana na hilo.

Madai ya Bw Kuria yanachukuliwa kuwa tu maoni yake kwani hakuna utafiti wowote uliofanywa kubaini kuwa kwa kweli ana umaarufu kiasi hicho Kisumu, wala kuorodhesha wanasiasa kulingana na umaarufu wao.

Hata hivyo, tangu Rais na Bw Odinga walipoafikiana, mbunge huyo amekuwa akizuru eneo hilo kinyume na awali, wakati kulikuwa na uhasama mkubwa kisiasa baina ya serikali ya Jubilee na upinzani.