HabariSiasa

Kuria sasa asajili TNA

April 28th, 2019 2 min read

Na NDUNGU GACHANE

MBUNGE wa Gatundu Kusini, Moses Kuria, amefufua kumbukumbu za chama cha The National Party Alliance (TNA), kwa kuunda chama chenye jina sawa atakachotumia kutetea masilahi ya eneo la Mlima Kenya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Chama hicho kwa jina Transformational National Alliance Party (TNA) kinalenga kuwapa hifadhi viongozi kutoka Mlima Kenya ambao wanahisi kuachwa yatima kufuatia kuvunjiliwa mbali kwa TNA mnamo 2016, kutoa nafasi kuundwa kwa chama cha Jubilee.

Vyama vingine 11 vilivyokuwa ndani ya uliokuwa muungano wa Jubilee, ikiwemo URP, pia vilivunjiliwa mbali.

Baada ya kuvunjiliwa kwa vyama hivyo, Rais Kenyatta naibu wake Dkt Ruto walitumia chama hicho kipya kushiriki uchaguzi mkuu wa 2017 na wakashinda baada ya kuendeleza kampeni za kulenga kuwaunganisha Wakenya.

Hata hivyo miaka miwili baadaye, mgawanyiko umeibuka ndani ya chama tawala cha Jubilee huku mirengo miwili ikiibuka; mmoja unaomuunga mkono Rais Kenyatta na mwingine unaoegemea upande wa Dkt Ruto.

Na hii ndio maana viongozi wa Mlima Kenya, wakiongozwa na Kuria wamesajili chama kipya ambacho wanatarajia kutumia kutetea masilahi ya eneo hilo katika serikali ijayo.

Maafisa wa chama hicho kipya ni; Mwenyekiti wa Kitaifa Wachira Keen ambaye alikuwa mwenyekiti wa Bodi ya Huduma za Maji ya Athi, Naibu wa Mwenyekiti ni Dkt Cyrus Njiru ambaye zamani alihudumu Katibu wa Wizara ya Biashara. Afisa mwingine wa kitaifa wa chama hicho ni Bw Yassir Noor.

Kulingana na Bw Keen, kuundwa kwa chama hicho kulichochewa na kuibuka kwa fulana za manjano, rangi ya kilichokuwa chama cha URP katika mkutano uliohudhuriwa na Dkt Ruto katika eneo la Banana, Kiambu.

“Kwa hivyo, tulionelea kuunda chama hiki ili kiwahudumie wale ambao hawako mrengo wa Tanga Tanga au Kieleweke,” alisema Keen.

“Kuna hisia kwamba, Naibu Rais, ambaye anaonekana kufufua chama, kwamba anaweza kuwafungia nje baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya wanaoonekana kuwa na ndoto za uongozi. Pia, huenda akawapuuza wale ambao wanasisitiza kuwa sharti Dkt Ruto abainishe kile ambacho atawafanyia watu wa Mlima Kenya namna Rais Kenyatta alivyofanya miaka ya 2013 na 2017, mtawalia,” akaongeza.

Chama cha Transformational National Alliance kinalenga kuwasajili viongozi 40 waliochaguliwa katika eneo la Mlima Kenya ambao hawajaonyesha kuegemea mirengo ya Kieleweke au Tanga Tanga.

Wao ni pamoja na Seneta Irungu Kang’ata (Murang’a), wabunge Kanini Kega (Kieni) Patrick Wainaina (Thika Mjini) kati ya wengine waliochaguliwa bungeni bila kufadhiliwa na vyama vya kisiasa.

Kulingana na Katibu wa chama hicho, Arnold Maliba, wanatarajiwa kutumia mitandao ya kitaifa iliyotumiwa na vuguvugu la “Mbele Iko Sawa” lililoendesha kampeni za Rais Kenyatta kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017. Kundi hilo liliongozwa na Bw Kuria.

“Tunalenga kusajili angalau wanachama 100 katika angalau kaunti 24 inavyohitajika na sheria ya vyama vya kisiasa. Ili kufikia lengo hilo marafiki wetu watatumia mbinu za kipekee za kuwavutia wafuasi katika ngazi za kaunti. Kufikia sasa wamefikia kaunti 11,” akasema Bw Maliba.